Friday, September 22, 2023

MWENGE WA UHURU WAPOKELEWA RASMI MKOANI SINGIDA


MKUU wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amepokea rasmi Mbio za Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoani Tabora na aliyekabidhi ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Batlida Briani.

Makabidhiano yamefanyika leo tarehe 22 Septemba, 2023 katika viwanja vya Malendi Wilayani Iramba mkoani humo.

Akipokea Mwenge wa Uhuru, Peter Serukamba amesema kuwa lengo kubwa la kupokea Mbio za Mwenge wa Uhuru ni kufanya uchechemuzi wa miradi pamoja kuhamasisha upendo, amani na ushirikiano.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kulia) akiupokea rasmi Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Batlida Briani mapokezi yaliyofanyika katika viwanja vya Malendi wilayani Iramba.

Serukamba akizungumza muda mfupi baada ya kupokea Mwenge wa Uhuru amesema kuwa utazindua miradi mbalimbali ikiwepo miradi mbalimbali ikiwemo ya sekta ya elimu, afya, miundombinu ya barabara, maji, miradi ya utunzaji wa Mazingira.

Akizungumzia miradi amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai 2022 hadi Septemba, 2023 miradi yenye thamani ya fedha kiasi cha Sh. Bilioni 223.9 imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Amebainisha miradi ambayo inatekelezwa katika Mkoa wa Singida na Wilaya zake ni pamoja na sekta ya Elimu, Afya, Utawala, Kilimo, Uwezeshaji wananchi kiuchumi, Barabara, Nishati na Maji.

Akizungumzia sekta ya Elimu amesema kuwa Jumla ya sh. Bilioni 34.08 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu ya elimu hususani ujenzi wa shule mpya za BOOST na shule mpya za Sekondari kupitia mradi wa SEQUIP pamoja na utoaji wa elimu bila malipo kutoka shule ya msingi hadi kidato cha nne.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Taifa, Abdalla Shaib Kalm akizungumza wakati wa mbio hizo za Mwenge wa Uhuru.

Kwa upande wa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Taifa, Abdalla Shaib Kalm amesema kuwa lengo la kukagua miradi hiyo ni kuhakikisha miradi inayotekelezwa inaendana na thamani ya fedha.

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikipambana kutafuta fedha kwa kwa ajili ya maendeleo hivyo ni jukumu la watendaji kuhakikisha wanasimamia miradi kwa thamani ya fedha inayotakiwa.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Fatuma Mganga akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa mkimbiza Mwenge Taifa wakati wa mapokezi ya mbio hizo mkoani humo.


Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akisoma taarifa ya miradi mbalimbali iliyotekelezwa  mkoani humo.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kushoto) akiteta jambo na mkimbiza Mwenge wa Uhuru Taifa Abdalla Shaib Kalm wakati wa mapokezi ya mbio za Mwenge wa Uhuru 2023.




Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Taifa, Abdalla Shaib Kalm (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Singida Martha Mlata wakati wa mapokezi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani Singida.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kulia) akimkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Wilaya ya Iramba Sulleiman Mwenda ili kuukimbiza wilayani humo.

No comments:

Post a Comment