Wednesday, June 07, 2023

Diwani atajwa kuchafua hali ya hewa Mitundu, RC Serukamba amvutia kasi.

Wananchi  na Diwani wa kata ya Mitundu Katika Halmashauri ya Itigi Wilayani Manyoni Mkoani Singida Patrick  Masanja  wamelalamikiwa na viongozi wa Serikali kukataa kushiriki nguvu kazi katika miradi ya  maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa  na Kituo cha Afya eneo hilo kwa sababu ambazo hazikuweza kufahamika mara moja.

Malalamiko hayo yametolewa leo na  Viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya hiyo Kemilembe Lwota mbele ya Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba kwamba wananchi wamekuwa wakikatazwa na Diwani huyo kushiriki nguvu kazi katika miradi  ya ujenzi wa madarasa na Kituo cha Afya cha kata hiyo jambo ambalo limesababisha gharama na muda wa ujenzi kuongezeka.

DC Kemilembe alisema siku za karibuni walitembelea miradi hiyo na kamati ya usalama ya Wilaya na Diwani huyo alikataa kushiriki ziara hiyo kwa kuwa malalamiko yalikuwa mengi dhidi yake kuhusu kuwakataza wananchi wa eneo hilo kushiriki ujenzi wa miradi.

Hata hivyo kamati ya siasa ya Wilaya nayo iletembemea eneo hilo na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi ambapo DC Kemilembe amesema walimpatia nafasi Diwani huyo kuwaeleza wananchi hao kushiriki nguvu kazi katika miradi hiyo na alikataa kuongea neno lolote.

Naye Mwemwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Manyoni Barnabas Moshi alieleza kwamba Diwani huyo amekuwa ni changamoto eneo hilo ambapo kamati ya siasa ilipopata malalamiko dhidi yake walikuja kufanya mkutano na wananchi na hakuonesha ushirikiano.

Aidha kwa upande wake Diwani huyo alijitetea kwamba ni kweli wananchi hao hawashiriki kwenye ujenzi wa miradi hiyo kwa sababu wanazozijua wao wenyewe lakini yeye hajawakataza huku Mwenyekiti wa Halmashauri ya Itigi akimhakikishia RC Serukamba kwamba mara kadhaa Diwani huyo amekuwa akiwakataza wananchi kufanya kazi katika Kituo cha Afya cha Mitundu.

Akimalizia mjadala huo Mkuu wa Mkoa amewataka viongozi wa Halmashauri kuongeza idadi ya mafundi na vibarua katika miradi hiyo ili miradi ikamilike ifikapo tarehe 20/6/2023 huku akiahidi bàadhi ya wananchi na waliokuwepo eneo hilo kwamba swala la Diwani huyo anaenda kutafakari ili kujua jambo la kufanya dhidi yake.

 Hata hivyo RC Serukamba ametoa pongezi kwa Wilaya kwa hatua ambayo miradi hiyo imefikiwa huku akiwasisitiza kukamilisha ifikapo tarehe 20/06/2023 na kuwataka kuhakikisha zahanati na vituo vya Afya kuanza kutoa huduma kwa wananchi ifikapo 1/7/2023.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA WAKATI WA ZIARA HIYO.



Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kushoto) akisisitiza ukamilishaji wa ujenzi wakati wa ziara hiyo.






Ziara ikiendelea

No comments:

Post a Comment