Tuesday, May 02, 2023

RC Serukamba aagiza Zahanati ya Masagi kufunguliwa

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba  ametoa siku tano (5) kwa Mkurungezi wa Wilaya ya Iramba na Mganga wa Wilaya hiyo kuhakikisha Zahanati ya Kijiji cha Masagi iliyopo Kata ya Mtoa inafunguliwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi ifikapo Jumatatu tarehe 8 Mei. 2023.

RC Serukamba ametoa agizo hilo wakati wa Mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi wa Kijiji cha Masagi ambapo wananchi hao walilalamika kukamilika kwa Zahanati hiyo lakini mpaka sasa haijafunguliwa huku Diwani wa kata hiyo, Samweli Ntumba akikiri kwamba wameshapokea vifaa tiba na thamani mbalimbali.


RC Serukamba amesema kwamba haoni sababu ya wananchi kuteseka kufuata huduma za Afya mbali na eneo hilo wakati Serikali imekamilisha ujenzi wa Zahanati na imeleta vifaa tiba hivyo, aidha amemuelekeza Mganga wa Wilaya kusimamia shimo la kichomea taka likamilike ili huduma ziendelee.

Sambamba na hilo RC amewagiza Waganga Wakuu wa Wilaya kuongeza usimamizi wa watumishi walioko chini yao ili waweze kufika kwenye vituo vyao vya kazi saa moja na nusu badala ya kufika saa nne kama ilivyoripotiwa na wananchi wa Iramba.

Aidha RC amekemea vikali tabia ya Wauguzi  na  Manesi ambao wamelalamikiwa na wananchi wa kata hiyo kwa kutoa lugha mbaya kwa wajawazito na watoto na kuagiza DMO kuwachukulia hatua zaidi ya kuwahamisha vituo vya kazi.

MATUKIO KATIKA PICHA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Masagi wakati wa Mkutano wa kusikiliza na kutatua kero uliyofanyika katika kata ya Mtoa Wilayani Iramba.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga akizungumza wakati wa Mkutano wa kusikiliza na kutatua kero uliyofanyika katika Kijiji cha Masagi kata ya Mtoa Wilayani Iramba.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda akizungumza wakati wa Mkutano wa kusikiliza na kutatua kero uliyofanyika katika Kijiji cha Masagi kata ya Mtoa Wilayani Iramba. 











No comments:

Post a Comment