Tuesday, April 18, 2023

VIJANA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA YA MIRADI YA SERIKALI

 

Vijana wenye ujuzi mbalimbali Mkoani Singida wametakiwa kutumia fursa ya uwepo wa miradi ya Serikali ya ujenzi wa vyumba 102 vya madarasa na matundu 116 ya vyoo maeneo mbalimbali mkoani hapo kama fursa ya kujipatia ajira.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Afisa vijana wa Mkoa huo Fredrick Ndahani alipokutana na makundi ya vijana hao katika ukumbi wa mikutano wa Kanisa Katoliki ulioko mjini Singida.

Afisa Vijana huyo amesema Serikali imetoa jumla ya Tsh. Bilioni 9.024 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa matundu ya vyoo, nyumba vya walimu na ukarabati wa shule hivyo vijana watumie miradi hiyo kuonesha uwezo wao.

Ndahani akiwa katika semina hiyo amesema vijana wasisubiri fursa ziwafuate bali wazitafute zilipo kwa kuwa hawezi kujulikana mtu bila ya kujitangaza huku akiwasisitiza kutumia fursa zinazotolewa na Serikali.

"Ombeni kazi katika miradi hiyo kwakuwa hakuna mtu atakaye jua kuwa fulani ni fundi bila ya wewe kutoka na kuonesha ujuzi ulionao kijana" alisema Ndahani

Aidha Ndahani amewaeleza vijana kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kutoa mikopo kwa vijana yenye masharti nafuu na ambapo mpaka jumla ya Shilingi Milioni 100.2 zimetolewa kwa vikundi vya vijana  katika Mkoa wa Singida.

Saimon Mandela ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutenga muda wa kuongea na vijana kwani vijana wengi hawajui fursa zinazotolewa na Serikali pamoja na Miradi inayoletwa ndani ya Mkoa ambayo vijana wanaweza kuomba na kupatiwa ajira.

Itakumbukwa kwamba mwishoni mwa mwezi wa pili Katibu Mkuu CCM Daniel Chongolo alipofanya ziara Mkoani Singida alitoa maagizo kwa vijana kutumia vyuo vya VETA kupata ujuzi na wenye ujuzi  watumike kutekeleza miradi ya Serikali badala ya kuagiza watu kutoka nje ya maeneo husika.


No comments:

Post a Comment