Katibu Mkuu CCM Daniel Chongolo ameagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakisha wanatoa cheti cha msamaha wa kodi wa ongezeko la thamani (VAT) kwa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kabla ya kumaliza ziara yake ili Mkandarasi wa Mradi wa Maji unaotekelezwa katika Kata ya Chikuyu Wilayani Manyoni Mkoani Singida aweze kukamilisha kazi hiyo.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati alipotembelea Mradi huo baada yakupata maelezo ya utekelezaji wa Mradi kutoka kwa Meneja wa RUWASA Mkoa Said Lukas, kwamba wanasubiri cheti hicho ili Mkandarasi aweze kuendelea na kazi, Cheti ambacho kingekamilika kwa muda wa wiki mbili hadi tatu zijazo.
Katibu Mkuu alieleza kwamba chama hakiwezi kuvumilia ucheleweshaji wa ukamilishwaji wa miradi ambayo wananchi wanauhitaji mkubwa kwa sababu ya watu wachache ambao hawakamilishi wajibu wao.
"Hatuwezi kuwa tunajadili vitu vidovidogo ambavyo havihitaji fedha kuvichukulia hatua na kuvitekeleza, hivi inaonesha kuna watu wapo katikati hawataki kutimiza wajibu wao na sisi hatupo tayari tunachotaka nikutoa huduma ya maji kwa wananchi" alisema Chongolo na kuongeza
"Tunajadili swala la certificate wakati Wizara ya Maji na TRA wote wanatumia Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, sasa nataka kabla sijaondoka Singida certificate iwe imefika" alimalizia Chongolo.
Hata hivyo Chongolo amemuelekeza Meneja huyo kuhakikisha vijiji vilivyopitiwa na bomba hilo kuhakikisha vinapatiwa maji.
Awali akitoa ufafanuzi wa taarifa ya mradi Said Lukas, alieleza kwamba mradi huo ukikamilika utagharimu Bilioni 12 na utafikia vijiji 11 vya Wilayani Manyoni.
Amesema Mradi huo ulianza Julai 2017 na unategemewa kukamilika Desemba 2023 na inategemewa kuwafikia wananchi zaidi ya Elfu 55 ambapo mpaka sasa jumla ya Bilioni 4.9 zimekwisha tumika.
Aidha amesema kwamba Mradi huo utakapo kamilika utaongeza hali ya upatikanaji wa maji kutoka asilimia 54 mpaka kufikia asilimia 84.
Hata hivyo Katibu Mkuu huyo atafanya ziara Mkoani Singida kwa muda wa siku sita (6) ambapo atakagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule, vituo vya afya, barabara, miradi ya maji pamoja na kuzungumza na wananchi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment