Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA )
wameshauriwa kuimarisha mifumo kuanzia chini kueleza umuhimu wa ufundi na faida
zake ili kuwavutia vijana wengi kujiunga katika vyuo hivyo.
Ushauri huo umetolewa leo na Katibu Mkuu CCM Taifa Daniel Chongolo,
alipotembelea ujenzi wa majengo ya Chuo cha VETA Ikungi na kusihi kutengeneza programu
ya kueleza umuhimu wa ufundi na faida zake ili kuongeza kipato na kuimarisha
dhana ya ujasiriamali.
Amesema kwa sasa Taifa lina vyuo vichache vya Serikali ambavyo
vinatoa elimu ya kati hivyo kusababisha watumishi kwenye mashirika mbalimbali
kushindwa kusimamia upatikanaji wa uzoefu kazini.
Chongolo alisema tunaweza kuwa na vyuo vingi vya VETA lakini
usipowekwa mfumo mzuri wa kuwafanya vijana waone umuhimu wa kujiunga na vyuo
hivyo tutajikuta tunabaki na majengo tu ambayo hayawanufaishi wananchi.
"Anzeni kutengeneza programu ya kwenda chini kwenye
shule za Sekondari ili kabla vijana hawajamaliza kueleza umuhimu wa ufundi, faida
zake na namna unavyoweza kuzifikia faida hizo," alisema.
Alisema Serikali katika miaka hiyo mitatu imekuwa ikitoa fursa ya mafunzo ya ufundi bure lakini jambo la msingi ni VETA kupata vijana wa kutosha wanaojiunga na vyuo hivyo.
Naye Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, John Mwanja, alisema
ujenzi wa chuo cha VETA Ikungi ulianza katika bajeti ya 2019/2020 ambapo hadi
sasa Sh. Bilioni 2.3 zimeshatumika katika ujenzi huo ambao utakamilika Aprili
mwaka huu.
Mwanja alisema ili chuo hicho kiweze kuanza kazi kwa ajili
ya kukamilisha ujenzi, Serikali imetoa Sh. Milioni 259 na kwamba kitakapoanza
kitaanza kutoa mafunzo ya kozi ndefu kwa wanafunzi 240 na wa kozi fupi kati
wanafunzi 250 hadi 900 kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment