WAKATI Mkoa wa Singida ukijiandaa na maadhimisho ya Siku yake
ambapo unatimiza Miaka 60 imeanzishwa kampeni ya upandaji miti ambapo jumla ya
miti 254,880 imepandwa tokea zoezi hilo lilipoanza tarehe 07 January 2023.
Zoezi hilo linatekelezwa kila siku ya Jumamosi ambapo kwa
wiki hii Wilaya mbili za Ikungi na Manyoni zilipanda idadi hiyo ya miti mbapo
Ikungi imepandwa miti 54,000 na Manyoni miti 200,880 toka kuanza kwa kampeni.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amewapongeza
wananchi wa Wilaya hizo na kuwataka kuzilinda na kuitunza miti hiyo ili iweze
kukua.
Akiongea na wananchi wa Wilaya hizo leo wakati wa zoezi la
upandaji miti lililoanzia katika mpaka wa Manispaa ya Singida na Ikungi
mpaka Kintiku mpakani mwa Dodoma na
Singida ambapo RC Serukamba amesema lengo la Mkoa ni kupanda miti Milioni tatu
kwa Mkoa mzima (3,000,000) kwa mwaka 2023.
RC Serukamba ameeleza kwamba miti hiyo inapandwa katika maeneo
ya kingo za Barabara kufuata bikoni zake, mashuleni Hospitalini, vyanzo vya
maji, majumbani na kwenye nyumba za ibada.
Aidha Serukamba ameagiza Wakuu wa shule kupitia Maafisa
Tarafa na kata kuhakikisha miche inapatikana mashuleni ambapo kila Mwanafunzi
atapatiwa miti minne wakapande nyumbani kwao.
Hata hivyo RC ametoa maagizo kwa wenyeviti wa Halmashauri na
Madiwani kuhakikisha wanatunga Sheria kali zitakazo wafanya wafugaji kuwa
makini na mifugo yao sambamba na kuweka faini kubwa kwa atakaye sababisha mfugo
kula miti hiyo.
Serukamba ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Ikungi
kuhakikisha wananchi wa Ikungi wanapunguza tabia ya ukataji miti hovyo na
uchomaji wa mkaa kwakuwa imeonekana eneo hilo ndilo athirika zaidi.
Akimalizia hotuba yake Mkuu wa Mkoa huo ameahidi
kuwakutanisha Wakuu wa Wilaya wote na mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali yanayojishughulisha
na uboreshaji wa Miche ili waweze kuisaidia halmashauri ambazo zina changamoto
hiyo.
Kwa upande wake DC wa Ikungi Jerry Muro amesema wameshaweka
mkakati kupitia Maafisa Tarafa na kata kuhakikisha kuwa wanapanda miti Milioni
moja na laki tano kwa Wilaya nzima.
Amesema Mpango huo utakamilika kwa kuanzisha vitalu vya miti
kila kata ambapo itakuwa rahisi kuisambaza kwa wananchi na kuzisimamia
kikamilifu.
Jerry Muro ameeleza changamoto ambayo inaweza kutokea ni
upungufu wa miche ambapo amemuomba Mkuu wa Mkoa huo kuharakishwa kuwakutanisha
na wadau wanaozalisha miti ili zoezi lisikwame.
Naye DC wa Manyoni Rahabu Mwagisa amesema wameweza kupanda miti 200,880 kwa kushirikiana na Taasisi ya Wakala wa misitu Nchini (TFS) na muitikio mzuri wa wananchi.
MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA ZOEZI LA UPANDAJI MITI
No comments:
Post a Comment