Friday, January 20, 2023

RC Serukamba atoa maagizo mazito kwa Wilaya ya Manyoni

 

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Manyoni imetakiwa kuchunguza mauaji ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara pamoja na vitendo vya ushirikiana vinavyohusisha kufukua maiti na kuchukua nguo za ndani na baadhi ya vitu vya thamani.

Maagizo hayo yametolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa  Singida Peter Serukamba wakati wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi wa Manyoni na Itigi ambapo wananchi hao walilalamikia mauaji yanayotokea karibu kila wiki huku marehemu wakiwa hawana nguo za ndani.

Aidha alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa mauji hayo OCD Mratibu wa Polisi Ahmad Makele alikiri uwepo wa mauaji hayo ambapo alisema tayari walishaanza uchunguzi na kuwakamata baadhi ya watuhumiwa kwa ajili ya upelelezi.

Hata hivyo RC Serukamba ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa Takukuru Wilayani hapo  kuichunguza migogoro ya ardhi na baadhi ya watumishi wa Hospitali ya Wilaya ambao wamelalamikiwa  kushindwa kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa na kutumia vilevi wakiwa kazini.

Pamoja na mambo mengine RC Serukamba amemuagiza Kamishna wa ardhi Mkoa wa Singida Shamimu Hoza kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama kupitia migogoro yote ya ardhi na kutoa  mapendekezo ambayo yanatakiwa kukamilika ifikapo tarehe 20 mwezi wa Pili 2023.

Aidha RC Serukamba amemtaka Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Manyoni Fadhili Chimsala kuendelea kutathmini na kumaliza migogoro ya mradi wa mashamba ya korosho ili kila mtu apate haki yake.


Mwisho


No comments:

Post a Comment