Maafisa wa ardhi, Watendaji wa Vijiji na Kata Wilayani
Mkalama wametakiwa kuacha vitendo vinavyosababisha migogoro ya ardhi ambayo
imetajwa kama chanzo cha umaskini kwa wananchi wa Wilaya ya Mkalama.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter
Serukamba alipokutana na wananchi wa Wilaya hiyo katika ukumbi wa mikutano wa
Halmashauri hiyo ambapo walimueleza kero nyingi zikiwemo za ardhi.
RC amewataka Maafisa ardhi, na Watendaji wa Vijiji na Kata
kuacha kushiriki vitendo vya uuzaji wa ardhi ambazo tayari zinaumiliki wa watu
wengine na badala yake wajikite kuwashauri wananchi kuhusiana na mambo ya
ardhi.
Aidha akiwa katika kikao hicho RC Serukamba alipokea kero 49
ambapo 43 zilikuwa zikihusisha migogoro ya mashamba na viwanja baina ya mtu na
mtu au mtu na Serikali ya kijiji ambapo Maafisa ardhi na Watendaji wa kata na
vijiji walikiri kuifahamu lakini hawakuweza kuitatua kwa namna yeyote ile.
RC Serukamba amesema wananchi wanategemea mashamba na
viwanja hivyo kufanya maendeleo ya kiuchumi lakini kupitia utendaji
usioridhisha wa viongozi hao wananchi wamekuwa wakipoteza mashamba yao na
kusababishiwa umaskini.
"Maafisa ardhi, Watendaji wa kata na vijiji msiwe
chanzo cha umaskini wa wananchi, watu wanataka kulima wengine wanataka kufanya
maendeleo lakini mnawakwamisha mnaposhindwa kuwatatulia shida zao"
Serukamba.
Kufuatia hali hiyo RC Serukamba amewagiza Watumishi
kutekeleza wajibu wao kikamilifu ambapo amesema kwa kufanya hivyo kutapunguza
kero za wananchi.
"Kila Mtumishi ajitafakari kwamba kuanzia Jumatatu
mpaka Ijumaa amefanya nini katika kutekeleza wajibu wake? Kwakuwa wapo watu
wanakuwepo kazini kila siku lakini hakuna anachokifanya" Serukamba
Hata hivyo RC Serukamba anaendelea na ziara yake ya kusikiza
kero za Wananchi na siku ya kesho itakuwa zamu ya wananchi wa Wilaya ya Ikungi.
"Tunaanza msako wa Wanafunzi ambao hawajaripoti mashuleni"- RC Serukamba
Maafisa Elimu na Wakuu wa Wilaya Mkoani Singida wametakiwa
kutumia muda wa Siku tatu kuanzia leo
kuhakikisha hakuna mtoto atakayebaki nyumbani wakati wengine wakiwa
shuleni.
Kauli hiyo imetolewa leo na
Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba alipokutana na Maafisa Elimu na Wakuu
wa Wilaya ili kujadili hali ya usaili wa wanafunzi mashuleni.
Amesema idadi ya Wanafunzi wa Sekondari walioripoti
mashuleni ni ndogo ikilinganishwa na wingi wa madarasa yaliyojengwa na Serikali
hivi karibuni hivyo ni jukumu la Maafisa elimu hao kuhakisha wanasakwa popote
walipo na wapelekwe shuleni.
RC Serukamba ameendelea kueleza kwamba ifikapo Siku ya Jumatatu
tarehe 23 January, 2023 anataka taarifa ya kutoka kila kata kuhusu wanafunzi
wangapi wamesajiliwa na wangapi bado na sababu za kutosajiliwa.
Aidha, ametoa wito kwa wazazi na walezi Mkoani Singida
kuhakikisha hakuna Mtoto aliyechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza
atakayebaki nyumbani.
"Nimejiridhisha kwamba hali ya usaiili wa wanafunzi wa
kidato cha kwanza inasuasua sana, Serikali imejenga madarasa ya kutosha, imefuta
Ada mashuleni lakini bado wapo wazazi hawawapeleki watoto wao shuleni hili
halitakubalika" Serukamba
Kwa upande wake DC wa Iramba Suleimani Mwenda amesema bado
katika Wilaya yake hali ya kujiunga na kidato cha kwanza unaenda kwa kusuasua jambo
ambalo waliamua kuchukua hatua kwa kuwaita wazazi na wanafunzi ofsini kwake ili
kuwasikiliza.
DC Mwenda anasema amebaini kwamba wapo wazazi wanaozuia
watoto kwenda shule ili waweze kujiunga na shughuli za kiuchumi za kulima
kuchunga mifugo na baadhi kutafuta ajira binafsi.
Mwenda amesema wanapenda kutumia mbinu zote zikiwemo kuwashawishi kutumia Dola kuwapeleka shule na kuwachukulia hatua wazazi watakao bainika kuwazuia watoto kwenda shule.
No comments:
Post a Comment