Friday, November 11, 2022

"Hakikisheni chumvi inayotumika inakuwa na Madini joto ya kutosha" Dorothy Mwaluko

Maafisa wa Afya na Lishe Mkoani Singida wametakiwa kutembelea mashamba yote ya chumvi yaliyopo Mkoani hapo na kupima chumvi inayovunwa ili kuona kiwango cha Madini joto yaliyomo.

Maagizo hayo yametolewa leo tarehe 11.11.2022 na Katibu Tawala wa Mkoa huo Mwl. Dorothy Mwaluko alipotembelea mashamba ya chumvi yaliyopo Sekenke kijiji cha Nkonkirangi Wilaya ya Iramba ili kuona kiwango cha Madini joto yanayopatikana katika bidhaa hiyo.

Aidha wataalamu wa afya na Lishe walipima chumvi na kubaini kwamba ina kiwango kidogo cha Madini joto ambapo ndipo Katibu Tawala huyo alipotoa maelekezo kwa wataalamu hao kuyapitia mashamba yote ya chumvi na kupima  viwango vya Madini joto na kuwataka  kuweka mpango wa kuongezea Madini hayo kabla ya kumfikia mlaji.

Mwaluko amewataka wataalamu hao kuanza kutoa elimu kwa wanunuzi wa chumvi hiyo juu ya umuhimu wa madini joto katika mwili wa mwanadamu.

Amesema wanunuzi ndio watakao saidia kuwaelimisha wateja wao kulingana na bidhaa watakayoihitaji.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Lishe wa Mkoa Christowela Barnaba amesema bidhaa hiyo ni muhimu kuongezewa madini joto ili kuepuka kupata ugonjwa wa  goita jambo ambalo linaweza kugharimu maisha ya mlaji.

Amesema pamoja na kukutana na wanunuzi wao wataendelea kutoa elimu kwa wavunaji na wachuuzi pamoja na viwanda kuhakikisha wanauza chumvi ambayo ina kiwango cha kutosha cha Madini joto.

Naye Afisa Afya wa Mkoa wa Singida Mgeta Sebastiani amefafanua kwamba mwananchi anahitaji kuwa na afya bora itakayomsaidia kuzalisha mali na kuongeza kipato na kueleza kwamba ukosefu wa Madini joto inaweza kusababisha kipato kinachopatikana kutumika kujitibia.

Mgeta amewashauri wavuna chumvi hao kutazama Afya zao kabla ya biashara na kuondoa imani potofu kwamba chumvi ikiongezewa madini joto inabadilika rangi na wateja wataikataa.

No comments:

Post a Comment