Saturday, January 22, 2022

Serikali yatakiwa kuendelea kutoa Elimu kwa Jamii ya Watumia Maji Ikungi

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe. Jerry Muro akiwahakikishia Kamati ya Siasa Mkoa uwepo wa maji safi na Salama walipokagua Mradi wa Maji katika kijiji cha Ulyampiti wilayani Ikungi hivi karibuni.

Wananchi Wilayani Ikungi Mkoani Singida wameaswa kuitunza miradi ya maji kwa ajili ya kufaidisha vizazi vya Sasa na vijavyo huku wakikumbushwa kutumia maji Safi na salama yatokanayo na miradi hiyo.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka Singida Mhe. Yohana Msita akizungumza wakati wa ziara hiyo

Hayo yamesemwa Januari 20, 2022 na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka Singida Mhe. Yohana Msita alipokuwa akikagua Ujenzi wa Mradi wa Maji uliopo Kijiji cha Ulyampiti katika Wilaya ya Ikungi.

Aidha, ziara hiyo ya siku mbili katika Wilaya ya Manyoni na Ikungi ya kamati ya siasa mkoa wa Singida ililenga kukagua miradi iliyojengwa kwa fedha za uviko 19, fedha zitokanazo na tozo za miamala ya simu pamoja na mapato mbalimbali ya Halmashauri.

“Sasa hivi changamoto sio upatikanaji wa maji, changamoto iliyopo ni wananchi kuyatumia maji, tuendelee kutoa elimu kwa wananchi. Tuone maji yapo na watumiaji wapo”. Alisema Yohana Msita


Kamati hiyo imewapongeza watendaji wa Halmashauri ya Wilaya Ikungi kwa usimamizi mzuri wa fedha zilizotolewa na Serikali ya awamu ya Sita katika kutekeleza miradi mbalimbali ambapo ikatoa wito kwa wananchi wa vitongoji 2 vya kijiji cha Ulyampiti na maeneo ya jirani kuutunza na kuulinda mradi huo kwa kuwa unatosheleza mahitaji ya maji kwa sasa na ya baadae.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha kiasi cha Tsh. 164,813,431.00 kwa ajili ya utekelezaji wa urefushaji wa mradi wa Maji Ulyampiti ambao umesanifiwa kuwahudumia wakazi 2,755 wa kijiji hicho. 

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kazi zote za Mradi zimetekelezwa kwa asilimia 100% na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa gharama nafuu.

Kamati ya Siasa mkoa wa Singida wakiambatana na Watendaji wa Serikali  kuelekea kwenye Mradi wa Maji uliopo Kijiji cha Ulyampiti wilayani Ikungi

Awali akisoma taarifa ya Mradi Meneja wa Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Ikungi Mhandisi Hopeness Liundi amesema Mradi umeanza kutoa huduma tarehe 16 Agosti 2021 na hakukuwa na changamoto zozote wakati wa utekelezaji wa mradi.

Ameeleza kuwa mradi huo utapunguza ajali zinazoweza kutokea wakati wa kutafuta maji katika umbali mrefu hususani wanapovuka barabara ya lami.

Akihitimisha hotuba yake Liundi, ameishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maji ambayo imejenga mazingira mazuri ya wanafunzi wa shule ya msingi Ulyampiti kuwa na muda mwingi wa kujisomea badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji atokapo shuleni.

Hata hivyo ziara hiyo ya Kamati ya siasa imefanyika katika wilaya mbili za Manyoni pamoja na Ikungi ambapo walikagua miradi ya Maji, Afya, Elimu (Madarasa), Miundombinu ya barabara, ujenzi wa nyumba za Watumishi, mikopo kwa vikundi ambapo kamati hiyo imeridhishwa na ujenzi ulivyofanyika na namna ambavyo watoto wamekuwa wakiendelea kusajiliwa katika mashule hayo.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA

Sehemu ya muonekano wa juu Mradi wa Maji Ulyampiti Wilaya ya Ikungi

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro (kushoto) akizungumza wakati wa ziara hiyo

Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Ahmed Kaburu, akisisitiza jambo juu ya utunzaji wa (mitambo) Mashine ya kusaga walipotembelea Mradi wa Vijana wa kijiji cha Matare kujionea kiwanda kidogo cha kusaga kilichowezeshwa fedha Sh. Milioni 4.5 zitokanazo na  mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo. Aidha ni mashine pekee inayotoa huduma ya kusaga katika kijiji hicho. 

Kamati ya Siasa ya Mkoa ikiwa ndani ya darasa kuwasalimu wanafunzi walioripoti katika moja ya Shule zilizojengwa kwa fedha za Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 Wilayani Ikungi.

Wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Singida, wakiendelea na ukagua ujenzi wa Shule Wilaya ya Ikungi

Moja ya Jengo la shule ya Msingi ambapo wanafunzi wamesharipoti wilayani Ikungi

No comments:

Post a Comment