Serikali Yatakiwa
Kuendelea Kutoa Elimu Kwenye Vikundi
Wasimamizi wa Vikundi vya Vijana wajasiriamali wadogo wadogo mkoani
Singida wametakiwa kuvishauri na kuvisaidia vikundi hivyo kwa kuangalia mipango
kazi yao kabla ya kuwakopesha ili fedha watakazozipata waweze kuzitumia vizuri
na kuwaletea maendeleo.
Maagizo hayo yametolewa Januari 20, 2022 na Mwenyekiti wa CCM
Mkoa wa Singida Alhaji Juma Kilimba
alipokuwa akikagua kikundi cha vijana kilichopo Iguguno katika wilaya ya
Mkalama kinachofahamika kwa jina la Iguguno Youth Group ambacho kinajishughulisha
na ufatuaji wa matofali na ufugaji wa kuku wa kienyeji.
Ziara hiyo ya kamati ya siasa imeingia siku ya pili ikiwa na
lengo la kukagua miradi iliyojengwa kwa fedha za uviko 19, fedha zitokanazo na
tozo za miamala ya simu pamoja na mapato mbalimbali ya Halmashauri.
Aidha Alhaji Kilimba amesema vikundi vyote vinavyokopeshwa
fedha za Serikali ni lazima vilelewe vizuri ili vikomae na kufikia kikomo na kupisha
vikundi vingine viweze kukua hivyo akawataka Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa
na Wilaya kuhakikisha wanawashauri na kuwaongoza hasa katika kipidi
wanapowakopesha fedha ili waweze kufikia
malengo yao.
“Ni lazima elimu
itolewe kwa wanakikundi wajue namna ya kuandika mahesabu ya mapato na matumizi
wapate elimu juu ya namna ya kupambana na majanga yanayoweza kujitokeza katika
biashara zao pamoja kuendeleza mitaji iweze kukua” alisema Bwana Kilimba.
Hata hivyo ameitaka Serikali kuvisaidia vikundi hivyo kupata
masoko ya bidhaa wanazozalisha kama sehemu ya kuwaunga mkono hali itakayosaidia
kushawishi vijana wengine kujiunga au kuanzisha vikundi mbalimbali vyenye
kuongeza ajira na vipato kwa vijana.
Awali akisoma taarifa ya kikundi hicho Bi Winifrida Innocent
katibu wa kikundi amesema Halmashauri ya Mkalama iliwakopesha fedha kiasi cha
Sh. Milioni 15 ambazo zilitumika kununua baadhi ya vifaa kama mashine ya umeme
na inayotumia mikono kwa ajili ya kufyatulia matofali, vibao pamoja na sement.
Aidha ameishukuru Halmashauri ya Mkalama kwa kuwa imekuwa
ikiwasaidia ushauri na wataalamu ambao wamekuwa wakiwatembelea mara kwa mara.
Hata hivyo ziara hiyo ya Kamati ya siasa imefanyika katika
wilaya mbili za Mkalama pamoja na Iramba ambapo walikagua miradi ya maji,
madarasa na kituo cha afya ambapo kamati hiyo imeridhishwa na ujenzi ulivyofanyika na namna
ambavyo watoto wamekuwa wakiendelea kusajiliwa katika mashule hayo.
Hata hivyo Mwenyekiti amesisitiza utunzaji wa miradi hiyo ili
iweze kusaidia vizazi vijavyo hasa katika vyumba vya madarasa na thamani zake
wakati kwenye miradi ya maji akiwataka wataalamu kuhakikisha maji yanasambazwa
karibu na makazi ya watu.
No comments:
Post a Comment