Monday, January 24, 2022

Wawili wauwawa wakidhaniwa ni Majambazi

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida ACP. Stella Mutabihirwa  akionyesha Silaha aina ya AK 47 iliyokamatwa kutoka kwa Majambazi wawili Apolo Issa (32) ambaye ni mkazi wa Puma na Abdi Masoud (45) mkazi wa Mnung’una Katika Manispaa ya Singida ambao walishambuliwa na wananchi wenye hasira kali tarehe 23/01/2022 majira ya saa 3:00 usiku.

Watu wawili  wanaohisiwa kuwa ni majambazi wamefariki dunia baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kali usiku wa tarehe 23 Januari 2022 Katika Kijiji na Kata ya Ihanja Wilayani Ikungi Mkoani Singida  baada ya kufanya jaribio la kupora Mali ya mfanya Biashara mmoja Katika Kijiji hicho.

Hayo yamesemwa leo tarehe 24/01/2022 na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida ACP. Stella Mutabihirwa alipokutana na Waandishi wa Habari ofisini kwake  kutoa taarifa ya mauaji hayo ya vijana walioshukiwa kuwa ni majambazi.

Kamanda huyo aliwataja Majambazi hao ni Apolo Issa (32) ambaye ni mkazi wa Puma na Abdi Masoud (45) mkazi wa Mnung’una Katika Manispaa ya Singida ambao walishambuliwa na wananchi wenye hasira kali tarehe 23/01/2022 majira ya saa 3:00 usiku.

Aidha amebainisha kwamba Majambazi hao wamekutwa na Silaha aina ya AK 47 moja na risasi tisa (9) huku wakiwa wanahalimbaya baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kali.

“Watuhumiwa walipofikishwa kituoni, walipekuliwa na mmojawapo aitwaye Apolo Issa katika begi lake alikutwa na Silaha aina ya AK 47 moja ikiwa na risasi tisa (9), huku hali zao zikiwa sio nzuri kutokana na kushambuliwa na wananchi ambapo mtuhumiwa Abdi Masoud alikuwa na jeraha kichwani eneo la kisogoni na mtuhumiwa Apolo Issa akiwa na jeraha kisogoni, usoni na mguuni” Alisema Kamanda wa Polisi

Kutokana na hali hiyo, watuhumiwa walikimbizwa katika hospitali ya Mkoa wa Singida kwa matibabu na walipofika hospitalini Daktari aliwachunguza na kuthibitisha kuwa wamefariki Dunia na ndipo miili yao kuhifadhiwa hospitalini hapo.

Amesema Majambazi hao walikuwa wakifanya jaribio la kupora mali katika duka la mfanyabiashara mmoja ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ihanja wilayani humo na kwamba watuhumiwa hao walifika katika duka la mlalamikaji majira ya saa 3:00 usiku na kuulizia kama anauza mapanga ambapo aliwajibu hauzi huku mmoja wao akiwa amevalia vazi la Hijabu sura na sauti ikiwa ni ya mwanaume

Akiendelea na taarifa yake Kamanda huyo akabainisha kwamba Mfanyabiaashara huyo aliingiwa na hofu jambo ambalo lilisababisha kupiga simu kituo cha polisi Ihanja na kutoa taarifa kwa viongozi mbalimbali wa Kijiji hicho ambapo wananchi waliamua kuwatafuta na kuwakamata watuhumiwa hao kwa lengo la kuwapeleka Polisi.

Hata hivyo imesemekana baada ya wananchi hao kuwakamata watuhumiwa waliweza kuturoka tena jambo ambalo liliweza kuwakasirisha wananchi hao na kuanza kuwashambulia kwa kutumia silaha mbalimbali za jadi na kuwadhibiti hadi walipofikishwa kituo cha Polisi.

Aidha, Jeshi la Police mkoani Singida limewataka wananchi wa mkoa huo kuacha kujichukulia sheria mkononi pindi wanapobaini uhalifu wa aina yoyote badalayake watoe taarifa kwenye vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake.

Hata hivyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linaendelea kuwasihi wananchi kuacha kujitafutia mali kwa njia zisizo halali bali wafanye kazi halali.

No comments:

Post a Comment