Thursday, September 30, 2021

Wakulima wadogo mkoani Singida kunufaika na mradi wa Kilimo Biashara


Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mhe. Rahabu Mwagisa wakati wa uzinduzi wa mradi wa Kilimo Biashara uliyofanyika jana katika ukumbi wa mikutano Social Singida mjini

Afisa maendeleo ya jamii wilaya ya Iramba Bi. Jane Ng'ondi akichangia hoja wakati wa mkutano huo.

Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa wilaya ya Manyoni Bw. Fadhili Chimsala akichangia hoja

Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa wilaya ya Iramba Bi. Marietha Kasongo akichangia hoja

Meneja wa SEMA na mratibu wa mradi wa Kilimo Biashara mkoa wa Singida Bw. Ivo Manyaku wakati wa uzinduzi wa mradi.

Meneja wa SIDO mkoa wa Singida Agnes Yesaya akiwasilisha moja ya mada wakati wa uzinduzi wa mradi wa Kilimo Biashara uliyofanyika jana Singida mjini 

Waandishi wa habari wakiwa kazini wakati wa mkutano huo
 
Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mhe. Rahabu Mwagisa (kushoto) akisoma bango lenye ujumbe maalumu wa uzinduzi wa mradi wa Kilimo Biashara (MABADILIKO YA SEKTA YA KILIMO ILI KULETA AJIRA ZENYE STAHA KWA WANAWAKE NA VIJANA TANZANIA)

Mkutano ukiendelea

Serikali kwa kushirikiana na baadhi ya Halmashauri za Wilaya   za Mkoa wa Singida imeahidi kushirikiana na  Shirika la SEMA  katika mradi wa Kilimo biashara ambao utasaidia  uboreshaji wa maisha ya wakulima wadogo, Kaya zao, na  Mnyororo wa thamani kupitia ukuzaji wa kipato, matumizi ya mbinu za kilimo bora  zenye kulinda na kuboresha mazingira

 Akiongea wakati wa kuzindua mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Rahabu Mwagisa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Manyoni amesema kupitia mradi huo wakulima wadogo watasaidiwa mnyororo wa thamani wa mazao ya  mahindi, mbaazi, mtama, na alizeti na kuunganishwa na masoko.

Rahabu amesema  mradi huo utasaidia uwepo wa ushirikiano baina ya  sekta binafsi, na kutengeneza ajira kwa watu wengi lengo likiwa ni kufanya Mkoa kuwa kituo cha ubora (center of excellence) katika kuboresha maisha ya wakulima wadogo.

Hata hivyo amesisitiza kwamba mradi utawanufaisha wakulima wapatao 6,000 ikiwa ni pamoja na kusaidia mnyororo wa thamani katika mazao mbalimbali ili wakulima wadogo waweze kuchagua zao linalofaa kwa mahitaji na kupanua wigo wa uzalishaji wa bidhaa.

Mradi huo utakuwa unatekelezwa  katika wilaya za Ikungi, manyoni na iramba ambapo wakulima wadogo wa mazao ya alizeti mahindi mtama na mbaazi watafaidika.

Aidha DC huyo amebainisha mradi huo utakuwa na jukumi la  upatikanaji wa chakula cha familia, udhibiti wa kifedha, na fursa za uwekezaji kupitia Vikundi vya Akiba, Wazalishaji na Vijiji vya Biashara kwa wakulima wadogo, wanawake na vijana; na kuwaunganishaji wakulima na taasisi mbali mbali za kifedha na bidhaa za huduma  za kifedha zinazopatikana .

 mradi mpya unalenga kuboresha maisha ya wakulima wadogo 6,000 katika Mkoa wetu kwa kuimarisha miundo ya kusaidia biashara na mnyororo wa thamani wa mazao ya mahindi, mbaazi, mtama, na  alizeti” Alikaririwa Rahabu

Aidha ameendelea kufafanua  kwamba Mradi huo umeanza kwa wakati muaafaka ambapo  Mkoa  wa Singida unatekeleza  mpango wa kukuza na uzalishaji wa zao la alizeti unaolenga kuongeza uzalishaji wa mafuta ya alizeti kutoka tani 90,000  hadi tani 242,500 sawa na 54% ya jumla ya uagizaji wa mafuta ya kupikia kitaifa.

Amesema kwamba mpango kamili wa uzalishaji wa alizeti utajumuisha washikadau anuwai wakiwemo wakulima wadogo, vyama vya ushirika, asasi za kiraia, wakulima wakubwa, Wizara ya Kilimo, na Sekta Binafsi.

Aidha DC huyo ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa utayari wao wa kuwajengea uwezo  Maafisa Ugani wa kilimo kwa kuwapa ujuzi unaohitajika na vifaa vya kufanya kazi ili kuwasaidia vya kutosha wakulima wa Alizeti ikiwa ni pamoja na kutoa ruzuku ya mbegu bora za alizeti kwa wakulima wadogo.

Matarajio ya uongozi wa Mkoa wa Singida na Wizara ya Kilimo katika utekelezaji wa  " Mpango wa uwezeshaji Uboreshaji wa Maisha ya jamii  kupitia mradi wa kilimo cha kibiashara” ni kwamba utainua uchumi wa wakulima wadogowadogo kupitia kuongezeka kwa tija ya mazao yatakayowezeshwa na mradi huu”. Alisema DC.Rahabu

Naye mratibu wa mradi huo Bw. Ivo Manyaku alisema mradi huo ni maalumu kwa vijana na wanawake na ni muendelezo wa vikundi vilivyokuwa vikitumika katika mradi wa awali wa kuweka na kukopa.

Vikundi hivyo vya kuweka na kukopa ndivyo tunavyovigeuza kuwa vikundi vya wakulima  ambavyo pia vitakuwa vikipata mikopo kutoka katika vikundi walivyoanzisha. Alisema Bw. Manyaku.

Aidha amebainisha kwamba mradi huo utawaunganisha wakulima na wafanyabiashara  wakubwa ili kupata mahitaji na aina ya mazao yanayohitajika sambamba na uzalishaji wenye ubora.

Hata hivyo wakulima wengi mkoani Singida wamekuwa wakiuza mazao yao yakiwa shambani  jambo ambalo limekuwa likiwasababishia hasara,  hivyo mradi huu utahakikisha kwamba wanaongeza thamani mazao yao kabla ya kuyauza.  Alisisitiza bwana Mnyaku

Mnyaku aliendelea kusema kwamba vikundi vya wakulima vya kuweka na kukopa  vitatumika pia katika kuwakopesha wakulima wakati wakiendelea kusubiri bei nzuri ya mazao yao.

Pamoja na mambo mengi mradi huo utaanzisha mashamba darasa na mashamba ya mfano ambayo yatatumika kama kielelezo cha mbegu na mbolea bora zitakazotumiwa na wakulima wa vijiji husika.

Amemalizia kwa kusema mradi utaanzisha maoneho ya vijijiji ya biashara ambapo yatakuwa ni makutano ya wakulima wa maafisa ugani, wakulima na wanunuzi ili kujadili mahitaji sahihi ya kilimo husika.

Mwisho

No comments:

Post a Comment