Jumla ya wanawake 54 wamefariki dunia kwa kipindi cha mwaka 2014 Mkoani Singida kutokana na matatizo ya uzazi huku tafiti zikionyesha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi vinaweza kuzuiliwa kwa asilimia 35 iwapo huduma za uzazi wa mpango zitazingatiwa.
Hayo yameelezwa katika hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Vicent Kone iliyosomwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida Wilbard Marandu wakati wa uzinduzi wa huduma za Mkoba za uzazi wa mpango zinazofadhiliwa na shirika la Marie Stopes.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida Wilbard Marandu akikata utepe wakati wa kuzindua gari litakalotumika kutoa huduma za mkoba za uzazi wa mpango Mkoani Singida.
Dokta Kone amesema kiwango cha utumiaji wa huduma za uzazi wa mpango kwa Mkoa wa Singida ni asilimia 19 kikiwa ni kiwango cha chini kikilinganishwa na asilimia 27 ya kiwango cha kitaifa.
Ameongeza kuwa imani potofu na taarifa zisizo sahihi zimewafanya watu wengi kuwa waoga wa kutumia njia za uzazi wa mpango na kuamini kuwa vifo vitokanavyo na uzazi husababishwa na imani zilizopitwa na wakati, huku wengine wakiamini kuwa na watoto wengi ni utajiri.
Kaimu Mkurugenzi wa Marie Stopes Tanzania Mwemezi Ngemera akizungumza na wakazi wa Ilongero kuhusu huduma za Mkoaba za Uzazi wa Mpango.
Kaimu Mkurugenzi wa Marie Stopes Tanzania Mwemezi Ngemera amesema huduma za mkoba za uzazi wa mpango zitatolewa bure kutokana na ufadhili walioupata kutoka Serikali ya Uingereza kupitia shirika la UKAID.
Ngemera ameongeza kuwa malengo ya huduma hizo za uzazi wa mpango ni kuiwezesha jamii kuchagua njia ya uzazi wa mpango in ayoihitaji hasa wakiwalenga vijana na kauli mbiu ya 'chagua maisha kwa kutumia uzazi wa mpango'.
Mrembo anayeshikilia taji la Miss Marie Stopes Doreen Benne akiwashauri vijana wa Ilongero Mkoani Singida kutumia njia za uzazi wa mpango.
Naye mrembo anayeshikilia taji la Miss Marie Stopes Doreen Benne amewahamasisha vijana na wanafunzi Mkoani Singida kutumia njia za uzazi wa mpango kwani zitawaepusha na mimba zisizotarajiwa na kukatisha ndoto zao.
Benne amesema mimba ambazo hazijapangiliwa huchangia vifo 1400 kila mwaka vikitokana na utoaji mimba usio salama na mamia ya wasichana wakifukuzwa shule hivyo utumiaji wa njia za uzazi wa mpango utawasaidia vijana kujiepusha na hatari hizo.
Wanafunzi kutoka shule mbalimbali Mkoani Singida wakisikiliza huduma za uzazi wa mpango.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida Wilbard Marandu
akizindua gari litakalotumika kutoa huduma za
mkoba za uzazi wa mpango Mkoani Singida.
No comments:
Post a Comment