Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Vicent Kone akipanda mti wa muharaka siku ya upandaji miti iliyofanyika Sekondari ya Nkinto, Wilayani Mkalama.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Vicent Kone ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia sheria ndogo walizojiwekea ili kutunza mazingira.
Dokta Kone ametoa agizo hilo siku ya upandaji miti Mkoani Singida huku akishauri utaratibu wa kupanda miti kumi kwa kwaya za vijijini na mitano kwa kaya za mijini kila mwaka usimamiwe ili kuukinga Mkoa na jangwa.
Amesema hadi sasa kuna vijiji 230 Mkoani vyenye misitu ya asili yenye jumla ya hekta 520,325.48, na kuwa tangu mwaka 2010 hadi 2014 ni miti 10,347,870 tu iliyopandwa sawa na asilimia 37 ya lengo la kupanda miti 27,500,000 Mkoani Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Vicent Kone akiwaelekeza wanafunzi wa shule ya Msingi Nkinto jinsi ya kupanda miti katika siku ya upandaji miti iliyofanyika Sekondari ya Nkinto, Wilayani
Mkalama.
Naye Afisa Usafi na Mazingira Wilaya ya Mkalama Amon Sanga amesema Wilaya imejipanga kuendeleza misitu 25 yenye ukubwa wa hekta 23,108 kwa kutumia mbinu shirikishi, na pia shilingi milioni kumi zimetengwa kwaajili ya ununuzi wa mbegu za miti zitakazo sambazwa katika shule, taasisi, na vikundi 70.
Sanga ameongeza kuwa kwa kipindi cha mwaka 2013 na 2014 miti 240,373 sawa na asilimia 68.7 ya lengo ilipandwa huku idadi ya taasisi zinazosiha mbegu za miti zikiongezeka kutoka 11 hadi 30 na miche 213,500 ikizalishwa.
Afisa Usafi na Mazingira Wilaya Mkalama Amoni Sanga akisoma taarifa ya Wilaya siku ya upandaji miti Mkoani Singida.
Aidha Afisa Maliasili Mkoa wa Singida Charles Kidua amesema kauli mbiu ya siku ya Upandaji miti mwaka huu ni 'kata mti panda mti' ambapo Mkoa umeteua Januari 15 kuwa siku ya upandaji miti kulingana na hali ya hewa ya Mkoa.
Kidua ameongeza kuwa mbinu zitakazo tumika katika kutoa msukumo wa Upandaji miti kimkoa ni pamoja na kila wilaya kutenga maeneo kwaajili ya ukarabati kwa upandaji miti.
Amesema maeneo hayo yatakua ni rasmi kwa upandaji na utunzaji miti, wananchi wataweza kushiriki katika upandaji na utunzaji miti, wataalamu watapata fursa ya kufanya tafiti katika maeneo hayo na yatakuwa chanzo kizuri cha kuni, nguzo na mbao kwa matumizi ya wananchi.
Afisa Maliasili Mkoa wa Singida Charles Kidua akisoma taarifa ya Mkoa, siku ya Upandaji miti Mkoani Singida.
Baadhi ya wadau wakipanda miti katika eneo la Sekondari ya Nkito Wilaya ya Mkalama siku ya upandaji miti. Miti 540 ilipandwa katika eneo hilo siku hiyo.
No comments:
Post a Comment