Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Vicent Kone akizungumza kwenye
ufunguzi wa kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika kwenye
ukumbi wa mikutano wa Social Training Centre mjini Singida
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dokta Parseko Vicent Kone, amewahimiza wananchi
waliojiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, wajitokeze na kushiriki kwenye
mikutano ya kampeni ili kujijengea mazingira mazuri ya kuchagua viongozi bora.
Dokta Kone ametoa wito huo jana wakati akifungua kikao cha kamati ya
ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Social
training centre mjini Singida.
Amesema mikutano hiyo ya kampeni ni mahali wagombea wa ngazi mbalimbali
za uongozi wanapotangaza sera zao hivyo basi hapo ndipo mahali pekee wananchi
wanaweza kujua uwezo wa uongozi wa mgombea na iwapo sera zake zinagusa
vipaumbele vyao.
“Nawasisitiza wananchi wajitokeze na kushiriki kwenye mikutano ya kampeni
kwa amani na utulivu na watoe taarifa mapema kwenye vyombo vya usalama
wanapohisi au kuona baadhi ya wananchi wakitaka kuvuruga amani au kutaka
kutekeleza vitendo vya uvunjifu wa amani”, amesema Dokta Kone.
Dokta Kone ameongeza kuwa matarajio ya wananchi ni kuwa uchaguzi wa
serikali za mitaa utafanyika kama ulivyopangwa na hatimaye kuwapata viongozi
ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa kwa amani na utulivu.
Katika hatua nyingine, Dokta Kone ametumia fursa hiyo kuwakumbusha
viongozi na watendaji kuhakikisha wanafunzi waliofaulu, wanajiunga na kidato
cha kwanza mwakani bila kukosa.
“Isitokee mwanafunzi kubaki nyumbani kwa kushindwa kuhudhuria shule
aliyopangiwa”, alisisitiza.
Aidha Dokta Kone ametoa takwimu za kilimo kwa msimu wa mwaka 2013/2014
ambapo kwa mazao ya chakula jumla ya tani 913,143 zimezalishwa ikilinganishwa
na lengo la kuzalisha tani 780,420, wakati uzalishaji wa mazao ya biashara umefikia
tani 363,005.
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha ushauri mkoa wa
Singida wakifuatilia ajenda za kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa
mikutano wa Social Training Centre mjini Singida.
(Taarifa
na Nathaniel Limu).
No comments:
Post a Comment