Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi wa wakuu
wapya wanne wa Mikoa, amewahamisha wengine sita na ameamua kuwa wengine watatu
watapangiwa kazi nyingine.
Taarifa iliyotolewa mjini Dodoma jioni ya leo, Jumatano, Novemba 5, 2014 na
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa, Wakuu wapya wa Mikoa ni
Bi. Halima Omari Dendego ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Ibrahim
Hamisi Msengi ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bi. Amina Juma Masenza
ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Bwana John Vianney Mongella ambaye
anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Taarifa inasema
kuwa kabla ya uteuzi wake Bi. Dendego alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dkt.
Msengi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Bi. Masenza alikuwa Mkuu wa Wilaya ya
Ilemela na Bwana Mongella alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Taarifa hiyo
inasema kuwa Wakuu hao wapya wa Mikoa wataapishwa kesho, Alhamisi, Novemba 6,
2014 saa saba mchana, Ikulu, Dar es Salaam.
Aidha, taarifa
hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ambao watapangiwa kazi nyingine ni Kanali
(Mst) Fabian Massawe wa Kagera, Dkt. Christine Ishengoma wa Iringa na Kanali
Joseph Simbakalia wa Mtwara.
Wakuu wa Mikoa
ambao wamehamishwa vituo vya kazi ni Bwana Magesa S. Mulongo ambaye anakwenda
Mkoa wa Mwanza kutoka Arusha, Dkt. Rehema Nchimbi ambaye anakwenda Mkoa wa
Njombe kutoka Dodoma, Bwana Ludovick John Mwananzila anakwenda Tabora kutoka
Lindi, Kepteni (Mst) Anseri Msangi anayekwenda Mkoa wa Mara kutoka Njombe na
Mhandisi Everist Ndikilo ambaye anakwenda Arusha kutoka Mwanza.
Wengine
waliohamishwa ni Luteni (Mst) Chiku A.S. Galawa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma kutoka Tanga, Dkt. Rajab Rutengwe ambaye anakwenda Mkoa wa Tanga kutoka
Katavi, Bi Fatma Mwasa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kutoka Tabora na
Bwana Magalula S. Magalula ambaye anahamishiwa Lindi kutoka Geita.
Taarifa hiyo
imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara,
Mbeya,Morogoro, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu watabakia
kwenye vituo vyao vya sasa.
Aidha, Rais
Kikwete amefanya uteuzi wa Wakuu wapya wa Wilaya, kuhamisha baadhi yao na
kutengua uteuzi wa baadhi.
Taarifa kamili
itatolewa na Waziri Mkuu baada ya kuwa wamepangiwa vituo vya kazi.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Vicent Kone ambaye amebaki kwenye kituo chake cha Mkoa wa Singida.
No comments:
Post a Comment