Monday, April 14, 2014

SINGIDA MANISPAA KUANDAA MASTER PLAN


MKUTANO MKUU WA WADAU WA MASHAURIANO YA UANDAAJI WA MPANGO WA JUMLA WA MANISPAA YA SINGIDA, 14 APRIL, 2014.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone akisoma hotuba yake katika ufunguzi wa Mkutano huo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone akiwa katika picha ya pamoja na kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya ya Singida, Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Queen Mlozi na upande wa Kushoto ni Mwenyekiti wa Mkutano huo Mathayo Hango.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko V. Kone ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kushiriki kikamilifu katika uandaaji wa mpango wa jumla (master plan) wa Manispaa ya Singida kwakuwa zoezi hilo linatambulika kisheria na pia mpango huo utamilikiwa na kutekelezwa na wadau hao.

Dkt. Kone ametoa wito huo leo asubuhi wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mashauriano ya Uandaaji wa Mpango wa Jumla (Master Plan) wa Manispaa ya Singida katika ukumbi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA).

Amesema wadau hao wakishirikishwa wataweza kuratibu shughuli za Taasisi zao kuingizwa katika mpango mkuu ili ziweze kuoanishwa na Mipango ya jumla ya Manispaa.

Dkt. Kone ameongeza kuwa ushirikishwaji na makubaliano ya pamoja yataondoa muingiliano wa utekelezaji wa miradi mbalimbali kama ya umeme, maji, mawasiliano na barabara.

Amesisitiza kuwa wadau wahakikishe mpango bora na wa mapema unapatikana ili kuelekeza matumizi bora ya ardhi katika Manispaa ya Singida kwa ajili ya maendeleo ya kizazi kijacho.

Kwa upande wao wadau wa Maendeleo wa Manispaa ya Singida wamekubaliana kwa pamoja kuwa uandaaji wa mpango wa Jumla utangazwe kwenye Gazeti la Serikali, Vijiji 17 vilivyoingizwa mjini vitangazwe kuandaliwa Mipango ya Jumla, Vijiji 17 vilivyo ndani ya mipaka ya Halmashauri vifutwe isipokuwa vijiji vilivyo katika Kata ya Mtamaa.

Pia wadau wameshauri Mwongozo utolewe na Wizara  ya Ardhi, ili vijiji vya Kata ya Mtamaa viandaliwe mpango wa matumizi bora ya ardhi na vijiji visajiliwe mipaka yake.



Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali.
 

Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Joseph Mchina akiwasilisha mada kuhusu uandaaji wa Mpango wa jumla wa Manispaa ya Singida.

No comments:

Post a Comment