Monday, October 06, 2025

RC DENDEGO AWAPA KONGOLE MABINGWA WA CECAFA,WAAHIDI MAKUBWA ZAIDI!

Septemba 5,2025,

 


Mkoa wa Singida unaendelea kung’ara katika tasnia ya michezo, huku Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Halima Dendego, akiahidi mageuzi makubwa yatakayoifanya Singida kuwa kinara wa michezo nchini.

Akizungumza katika hafla maalum ya kuipongeza timu ya Singida Black Stars SC kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la CECAFA Kagame Cup 2025, RC Dendego alisema Serikali ya Mkoa imejipanga kuboresha miundombinu ya michezo, hasa viwanja, ili kuzalisha vipaji na kuviwezesha klabu nyingine kufikia mafanikio ya kimataifa.

“Singida tunalenga kupokea vikombe vingi zaidi. Tutaimarisha viwanja kama Bombadia ili kuwa fursa kwa timu zote za mkoa kujiandaa kisasa na kushindana kitaifa na kimataifa,” alisema RC Dendego huku akipongeza ari ya vijana wa Singida Black Stars.

Katika tukio hilo lililofanyika kwenye uwanja wa Bombadia, viongozi wa Mkoa, Manispaa, na Halmshauri mbalimbali walijitokeza kuipokea kwa shangwe timu hiyo iliyorudi na kombe la kihistoria, ikiwa ni timu pekee inayowakilisha mkoa huo katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.

RC Dendego aliwahakikishia wachezaji kuwa wataendelea kupewa motisha na zawadi zaidi endapo wataendeleza ushindi, akibainisha kuwa mafanikio yao ni sehemu ya ndoto kubwa ya kuifanya Singida kuwa "Jiji la Michezo."

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Godwin Gondwe, alisisitiza kuwa ofisi yake iko tayari kuendelea kushirikiana kwa karibu na timu zote za michezo ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa mfano wa mafanikio katika mkoa wa Singida.

Aidha, viongozi wa Singida Black Stars SC waliipongeza Serikali ya Mkoa kwa mapokezi na zawadi walizopewa, wakiahidi kuongeza juhudi kuhakikisha timu inakuwa tishio barani Afrika.























 


KWA YALIYOJIRI...TAZAMA VIDEO IFUATAYO HAPA CHINI👇







No comments:

Post a Comment