
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amewasisitiza wafanyabiashara wadogowadogo kutumia vizuri fursa za kidijitali kwa manufaa ya kukuza biashara zao na kuongeza kipato, akibainisha kuwa teknolojia ni nyenzo muhimu ya kufikia masoko mapya kwa haraka na kujifunza mbinu za kibiashara kwa vitendo.
Amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Wafanyabiashara Ndogondogo Mkoa wa Singida lililofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, ambapo alihudhuria kama mgeni rasmi.
Dkt. Fatuma Mganga alieleza kuwa wafanyabiashara wadogowadogo ndio nguzo ya uchumi wa Mkoa wa Singida na wanapaswa kupewa kipaumbele kuwa wafayabiashwara kuwa na mvhango mkubwa kwa taifa zima.
“Serikali na sisi mkoani hapa tunatambua kundi hili katika ukuaji wa uchumi. Ninyi ndio mnaochachusha na kuuchangamsha uchumi wa Singida, hivyo tunawathamini na kuwapa kipaumbele,” alisema.
Aidha, alihimiza kila mfanyabiashara kuhakikisha anajisajili na kupata kitambulisho cha mjasiriamali ili aweze kunufaika na mikopo iliyotengwa na serikali.
“Tuhakikishe kila mmoja wetu anacho kitambulisho chake. Hakuna tajiri ambaye ameajiriwa; kila tajiri ni mfanyabiashara au mjasiriamali. Hivyo, ninyi ni watu muhimu sana katika kukuza uchumi wa mkoa wetu,” alisisitiza
Kwa upande wake Bi. Donatila Vedasto, Katibu Tawala Msaidizi wa Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji mkoa wa Singida, alisema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwaunganisha wafanyabiashara wadogowadogo na kuhamasisha usajili ili kujikwamua kiuchumi na kutambulika na serikali Pamoja na kupata fursa za mikopo kwa haraka.
“Kwa sasa tuna zaidi ya wafanyabiashara wadogowadogo 15,000 katika halmashauri saba, wengi wao wakiwa Manispaa ya Singida. Ili wanufaike na mikopo, lazima wawe na vitambulisho vya mjasiriamali,” alisema.
Bi.Vedasto aliongeza kuwa nidhamu ya fedha ni msingi wa maendeleo ya biashara. “Biashara haina ubia na mtu binafsi. Ukivitenganisha, unasonga mbele. Lakini ukivichanganya, unakwamisha maendeleo,” alisema.
Aidha Mratibu wa Wafanyabiashara Wadogowadogo Mkoa wa Singida, Bi.Irene Beichumila, alieleza kuwa hadi kufikia 30 Agosti 2025, jumla ya vitambulisho 880 vimesajiliwa na zaidi ya shilingi milioni 100 za mikopo zimelipwa kwa wanufaika kupitia Benki ya NMB. Hata hivyo, alibainisha changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara kushindwa kulipia vitambulisho licha ya kujisajili.
Baadhi ya washiriki walitoa maoni yao baada ya kongamano hilo. Semeni Chamleta Gamwai, msafirishaji bodaboda, alisema amejifunza umuhimu wa mikopo, usajili na bima. Havijawa Omary, Mwenyekiti wa Umoja wa Mama Lishe Tanzania (UMALITA), alisisitiza kuwa makongamano hayo yanawapa wanawake nafasi ya kujikita zaidi kwenye fursa za biashara. Naye Abiud Mlowezi, Katibu wa Maafisa Usafirishaji (bodaboda), alisema wameona matumaini mapya ya maendeleo kutokana na maeneo yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya biashara.
Kongamano hilo liliambatana na mada mbalimbali kutoka taasisi za NMB, TRA na NSSF, ambapo wafanyabiashara walipata elimu ya huduma na mikakati ya kuimarisha mitaji. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa biashara ndogo ndogo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa wa Singida, huku mwakilishi wa wizara ya Maendeleo ya jamii aliupongeza mkowa wa Singia kwa hatua hii kubwa ya kongamano hilo.
No comments:
Post a Comment