Thursday, May 22, 2025

UKAGUZI WA MIRADI WILAYANI IKUNGI,UTEKELEZAJI UNAENDELEA!

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego ameongoza ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Ikungi leo Mei 22,2025 katika Wilaya ya Ikungi ili kufahamu juu ya itekelezaji wa miradi mbali mbali inayotelelezwa na fedha kutoka Serikali kuu kadhalika na mapato ya ndani ya Halmashauri.

Katika ziara hiyo Mhe.Dendrgo ameambatana na viongozi mbali mbali akiwepo  Katibu Tawala wa Mkoa Dkt. Fatuma Mganga,wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Ikungi,Wakuu wa idara na vitengo,Sekretarieti ya Mkoa,waratibu wa mwenge na wananchi kutoka Wilayani Ikungi ikiwa ni maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu Julai 2025.

Miradi iliyokaguliwa inagusa sekta muhimu zikiwemo elimu, maji, afya, miundombinu ya barabara, vijana, na utawala. Miradi hiyo imepangwa kutembelewa au kuwekewa mawe ya msingi na Mwenge wa Uhuru kwa mujibu wa mpango wa kitaifa wa kuhamasisha shughuli za maendeleo katika jamii.

Katika sekta ya elimu, viongozi hao wametembelea mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Samamba (Utaho 'A') unaogharimu shilingi 544,225,626 fedha zilizotolewa na Serikali Kuu. Mradi huu umepangwa kuwekewa jiwe la msingi kutokana na mchango wake mkubwa katika kupanua fursa za elimu kwa vijana wa maeneo ya Utaho na jirani.

Kwa upande wa maji, ukaguzi umefanyika katika mradi wa maji wa Utaho 'A' unaogharimu shilingi 300,000,000, ukitekelezwa kwa ufadhili wa wahisani. Aidha, mradi mwingine wa maji eneo la Wibia umehusishwa pia, wenye thamani ya shilingi 60,000,000 ukifadhiliwa na Serikali Kuu. Miradi yote hii inatarajiwa kuwekewa mawe ya msingi na Mwenge wa Uhuru.

Katika sekta ya afya, ujenzi wa walkways katika Hospitali ya Wilaya ya Ikungi umeangaliwa kwa makini. Mradi huo wa thamani ya shilingi 195,000,000 umetekelezwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu na utatembelewa na Mwenge wa Uhuru kama sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya huduma za afya kwa wananchi.

Miradi ya barabara pia imechukua nafasi muhimu, ambapo barabara inayosimamiwa na TANROADS pamoja na ile mpya ya TARURA zimetembelewa ili kuhakikisha maandalizi yanaendelea kwa kasi na ubora unaotakiwa kabla ya ujio wa Mwenge wa Uhuru.

Kwa upande wa maendeleo ya vijana, viongozi hao wametembelea mradi wa Kikundi cha “Ikungi Boys” ambao umetekelezwa kwa gharama ya shilingi 10,000,000 kwa mchango wa Halmashauri. Mradi huu unaonyesha namna vijana wanavyoweza kushirikishwa katika uchumi kupitia mikopo na shughuli za kiuchumi zinazowezesha kujiajiri.

Katika eneo la utawala, ujenzi wa jengo la ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeangaziwa, mradi unaogharimu shilingi 263,075,564.14 ukiwa umefadhiliwa na Serikali Kuu. Jengo hili pia limepangwa kuwekewa jiwe la msingi kutokana na umuhimu wake wa kuboresha huduma za kiutawala na usimamizi wa rasilimali misitu.

Akizungumza baada ya ukaguzi, Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego amesema: “Miradi ni mizuri, huduma kwa wananchi na mradi ni kitu cha msingi. Mwenge ni shughuli pevu hivyo tunatakiwa kufanya kazi kwa nguvu zaidi. Barabara zote mbili ziendelee na ujenzi — ile ya TANROAD na hii mpya ya TARURA.” Aidha, amesisitiza kuwa miradi hii iendane na mahitaji ya wananchi waliopo katika eneo husika ili iwe na tija na kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya jamii.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt. Fatuma Mganga, amesema: “Miradi yote ni mizuri, haswa shule ni nzuri. Cha msingi katika miradi hii ni kuhakikisha zirekebishwe sehemu zenye mapungufu. Pia nasisitiza suala la upandaji wa miti kwenye miradi, ni jambo la muhimu ili kuboresha mazingira yetu.”

Mwenge wa Uhuru ni alama ya mshikamano, amani na maendeleo. Kabla ya kufika kwenye Halmashauri husika, ni utaratibu wa Serikali kuhakikisha kuwa miradi yote itakayopitiwa imekaguliwa kwa kina ili kuangalia ubora, thamani ya fedha na mchango wake katika maendeleo ya wananchi.

Mkoa wa Singida umeweka mkazo wa kuhakikisha miradi yote inayoandaliwa kwa ajili ya Mwenge inatekelezwa kwa viwango, kwa wakati na kwa uwazi ili kuwahudumia wananchi ipasavyo.

Ukaguzi wa miradi katika Wilaya ya Ikungi umeonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Mkoa wa Singida katika kusimamia maendeleo ya wananchi kupitia miradi ya afya, elimu, maji, vijana na miundombinu. 

Uongozi wa Mkoa umeendelea kuhimiza uwajibikaji, usimamizi makini na uboreshaji wa mazingira katika maeneo yote ya miradi kabla ya kuwasili kwa Mwenge wa Uhuru, kama ishara ya uwazi na uzalendo katika maendeleo ya Taifa.

















No comments:

Post a Comment