Monday, June 03, 2024

RC SINGIDA – TUTAKWAMUA HARAKA UJENZI WA MAJENGO YA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA SINGIDA ‘MANDEWA’ ULIOKWAMA ILI WANANCHI WAWEZE KUPATA HUDUMA ZA AFYA.

Mkuu wa mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego ameahidi kushughulikia kwa haraka mkwamo wa ujenzi wa majengo Matatu (3) katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida iliyopo Kata ya Mandewa katika Manispaa ya Singida, jengo la ghorofa Tatu linalotarajiwa kutoa huduma za kibingwa ikiwemo upasuaji wa mifupa, wodi za watoto, huduma za wagonjwa mahutututi, maabara na huduma za ufamasia. 

Jengo hilo la ghorofa Tatu ujenzi wake ulianza mwaka 2014 na kusimama kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo Mkandarasi aliyekuwa anajenga jengo hilo kusimamishwa kuendelea na ujenzi kutokana na uwezo mdogo katika utekelezaji wa mradi huo.

RC Dendego ametoa kauli hiyo katika kikao na Watumishi wa Hospitali hiyo cha kusikiliza  kero na kukagua majengo ambayo ujenzi wake umesimama na kusisitiza kuwa  atalibeba jambo hilo na kulifanyia kazi ili ujenzi huo uweze kuendeleo na kukamilika kwa haraka lengo likiwa ni kuongeza utoaji wa huduma za matibabu kwa wananchi karibu na maeneo yao.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego (watatu kutoka kushoto), akisisitiza jambo wakati akizungumza na Watumishi wahudumu wa Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida Martha Mlata, Katibu wa CCM mkoa wa Singida Lucy Boniface na Mkuu wa Wilaya ya Singida Godwin Gondwe (kushoto kwa Mkuu wa Mkoa).

“Mimi ni Muumini ya Namba Moja kwa kila jambo hivyo nataka Hospitali hii ya Rufaa ya Mkoa iweze kushika Namba 1 nchini na Dunia kwa ujumla kwa utoaji huduma za kiwango cha juu za afya kwa wananchi kwani Hospitali nyingine wanaweza kwa nini sisi tushindwe na Serikali imewezesha vifaa na Watumishi wapo” Amesisitiza RC. Halima Dendego.

Kuhusu Watumishi wanaojitolewa kwa muda mrefu bila kupata ajira, Mkuu huyo wa mkoa ameutaka Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kumpatia orodha ya Watumishi wote wanajitolewa lakini hawajapata ajira ili aweze kuwasaidia katika ngazi husika.

Hata hivyo, Mhe. Dendego amewapongeza Watumishi hao kwa kufanya kazi kwa bidii bila kukata tamaa kutokana na kutopatiwa ajira na kusisitiza kuwa jambo hilo atalishughulikia ili watumishi hao waweze kupata ajira za kudumu.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida Martha Mlata, akisisitiza jambo kwenye kikao kifupi mara baada ya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida iliyopo kata ya Mandewa Singida Mjini. Juni 3, 2024

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida Martha Mlata, amewasisitiza Watumishi wa Hospitali mkoani humo kuendelea kuchapa kazi bila kuchoka kwa viwango vya juu kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita inawajali na itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa muda muafaka.

Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida Dkt. David Mwasota ameishukuru Serikali kwa kuwa bega kwa bega na Watumishi wa afya ikiwemo kuwapatia vitendea kazi vya kisasa na kuboresha maslahi yao hivyo jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi ili wasiende mikoa mingine kufuata huduma hizo za afya.

Mkuu wa Mkoa wa Singida akiongoza zoezi la ukaguzi wa Majengo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida iliyopo Kata ya Mandewa Singida Mjini Juni 3, 2024

Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe. Godwin Gondwe, akizungumza kwenye kikao kifupi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida kuzungumza na Watumishi wa Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida iliyopo Kata ya Mandewa Singida Mjini Juni 3, 2024 

Katibu wa CCM mkoa wa Singida Lucy Boniface, akizungumza jambo kwenye kikao kifupi mara baada ya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida iliyopo kata ya Mandewa Singida Mjini. Juni 3, 2024

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mandewa Dkt David Mwasota akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Hospitali hiyo kwa Mkuu wa mkoa wa Singida.



Kikao kikiendelea

No comments:

Post a Comment