Tuesday, February 06, 2024

RC SERUKAMBA: SINGIDA ITAWEZA KUINGIA KATIKA RAMANI UZALISHAJI NCHINI IWAPO MAAFISA KILIMO MTAWAJIBIKA

 MKUU wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, amewataka Maafisa Kilimo Mkoani Singida kuweka mkazo katika kuwaelimisha wakulima umuhimu wa kutumia mbolea na mbegu bora kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao ili mkoa huu uweze kuingia katika ramani ya uzalishaji nchini.

Alisema hayo Februari 5, 2024 wakati wa kikao kazi cha kupokea taarifa ya hali ya usambazaji wa mbolea na mbegu za alizeti zenye ruzuku ya Serikali katika Halmashauri ambacho kiliwashirikisha Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Kilimo, taasisi mbalimbali za Mkoa wa Singida, viongozi wa Dini na baadhi ya wawekezaji wenye viwanda Mkoani humo.

“Kazi yenu Maafisa kilimo ni kwenda kuongea na wakulima na kuwaambia kuna umuhimu wa kutumia mbolea, umuhimu wa kutumia mbegu sahihi umuhimu wa kulima sawa sawa, kuhakikisha mnapima afya ya udongo ya kila mkulima ili muwaeleze shamba lako hili unatakiwa utumie mbolea kiasi hiki, tukifanya hivyo niwahakikishie Singida itaingia kwenye ramani ya uzalishaji wa nchi hii,” alisema Serukamba.

Serukamba alisema kama hakutakuwa na matumizi sahihi ya mbolea na mbegu bora Mkoa wa Singida tutabakia kusikiliza yanaingia sikio hili na kutoka sikio jingine na kilimo kinabaki kuwa kile kile kwa kila msimu.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema Serikali inajitahidi sana kuwekeza kwenye kilimo katika Mkoa wa Singida ambapo inaleta mbegu za alizeti ambazo karibu zote zinazozalishwa na Wakala wa Taifa wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mbegu za Kilimo (ASA) zinaletwa Singida.

“Leo hii kuna zaidi ya miradi mikubwa ya umwagiliaji na mingine ipo njiani inakuja ambayo itagharimu zaidi ya Sh. Bilioni 50, kama Serikali inawekeza kiasi hiki katika mkoa wetu halafu Maafisa Kilimo hatuwasaidii wakulima wajue mbinu bora za kilimo umaskini unaondokaje,” alihoji Serukamba.

Serukamba aliongeza kuwa ili kuhakikisha Maafisa Ugani wanawajibika vyema na kazi zao, amewagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani Singida kuwapima kwa vigezo vinne (4) kama wanafiti katika nafasi hizo walizonazo.

Vigezo hivyo ni kama wanatembelea wakulima wengi, wanahamasisha matumizi ya mbolea kwenye maeneo yao, ugawaji wa mbegu za alizeti na nne ni kama wamepima mashamba mangapi kujua afya ya udongo.

“Rais ametuletea pikipiki 195 Mkoa wa Singida na kila Afisa Ugani ana pikipipiki, hivyo hana sababu ya kutotembelea wakulima mnataka nini, naombeni nendeni mkatekeleze wajibu wenu,” alisema Serukamba.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, alisema ili kuweza kubaini eneo gani kuna upungufu wa utoaji wa mbolea na mbegu, Maafisa Kilimo wafanye utafiti wa kila kijiji na kata na maeneo ambako pembejeo hizo hazijafika mikakati ya kupeleka ifanyike haraka.

“Tukishabaini kijiji au kata fulani bado mbolea na mbegu haijafika Mwenyekiti wa kijiji husika aitishe mkutano wa wananchi kuwaeleza mbolea na mbegu zinapopatikana.


No comments:

Post a Comment