MKUU
wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amewagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za
Wilaya mkoani hapa kuziondoa kwenye akaunti za halmashauri na kuzihamishia
kwenye miradi husika zaidi ya Sh. bilioni 5 zilizotolewa na Serikali ili
utekelezaji wa ujenzi wa miradi hiyo uanze haraka.
Ametoa
agizo hilo leo (Januari 29, 2024) katika
kikao cha kufanya tathimini ya maendeleo
ya zoezi la uandikishaji watoto wanaojiunga na shule za awali, darasa la
kwanza na kidato cha kwanza ambacho kiliwashirikisha Wakuu wa Wilaya,
Wakurugenzi, Maafisa elimu kutoka halmashauri zote za mkoani Singida.
"Tumepewa
siku 90 kukamilisha ujenzi wa miradi kutokana na fedha hizi tulizoletewa, kwa
hiyo naomba fedha zote ziondoke kwenye halmashauri ziende kwenye miradi husika
ili utekelezaji wa ujenzi uanze mara moja," alisema Serukamba.
Aidha,
Mkuu huyo wa Mkoa alisisitiza kuwa Wakurugenzi wote wanatakiwa kuonyesha fedha
zote walizopata na kuainisha miradi gani wanakwenda kuitekeleza ili wananchi wa
maeneo husika waweze kunufaika na matunda ya Serikali yao kwa kupata huduma stahiki
katika maeneo yanayowazunguka.
Naye
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dk. Fatuma
Mganga alisema Sh. milioni 350 zilizopelekwa katika Halmashauri ya Wilaya ya
Manyoni zitumike kumalizia ujenzi wa bwalo katika Shule ya Wasichana ya Solya
ili wanafunzi wa kidato cha tano na sita watakapoanza masomo wasipate tabu.
No comments:
Post a Comment