Sunday, December 31, 2023

RAIS DKT. SAMIA ATOA ZAWADI ZA MWAKA MPYA KWA WATOTO YATIMA MKOANI SINGIDA

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassani ametoa zawadi  mbalimbali za upendo vikiwamo vyakula kwa vituo viwili vya kulelea watoto yatima na waishio katika mazingira magumu vilivyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida kwa ajili ya kuukaribisha mwaka mpya 2024 ambapo watoto hao wamemshukuru Rais kwa zawadi hizo.

Vitu vilivyotolewa kwa vituo vya Malaika wa Matumaini na Amani Center for street Children ambavyo vimekabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba kwa niba ya Rais ni mchele, mbuzi, maharage, sukari, sabuni, unga wa sembe na mafuta ya alizeti.

Akizungumza baada ya kukabidhi zawadi hizo, Serukamba alisema ni dhamira yake ya dhati ya Rais kuungana na watoto yatima na waishio katika mazingira magumu mkoani Singida na anawapenda watoto wote na anaungana nao katika kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kushoto), akizungumza na Watoto wanaolelewa na Kituo cha watoto cha Malaika wa Tumaini wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya zawadi ya mwaka mpya kutoka kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Nipende kuwapongeza na kuwashukru Masista pamoja na Wadau wengine ndani ya Mkoa wa Singida kwa jitihada zao katika kuyahudumia makundi yenye uhitaji, juhudi hizi zinadhihirisha wazi kuwa wadau na jamii kwa ujumla wanavyounga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha makundi hayo yanapata afya, elimu, chakula, mavazi na malazi" alisema.

Serukamba alitoa wito kwa wadau na jamii ndani na nje ya mkoa wa Singida kwa upendo kuungana na Rais Samia kuendelea kuwakumbuka wenye uhitaji wakati wote.

Naye Mkuu wa Kituo cha kulelea watoto cha Malaika wa Tumaini, Sista. Frola Phaustine, alimshukru Rais Samia Suluhu Hassan kwa msaada huo na kwamba ameonyesha dhahiri upendo wa dhati kwa Watoto yatima.

Kituo cha Malaika wa Matumaini kina watoto yatima 48, ambao wote wamekuwa wakipatiwa elimu ya awali, msingi, sekondari na ufundi, kwa lengo la kuwajenga wanafunzi wanaohitimu hapo, kuweza kumudu maisha yao ya baadae.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, akiteta jamba na mtoto anayelelewa na Kituo cha watoto cha Malaika wa Tumaini mara baada ya kukabidhi zawadi ya mwaka mpya kutoka kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Watoto wanaolelewa katika kituo cha Amani Center for street Children kilichopo katika Manispaa ya Singida wakipokea zawadi za mwaka mpya 2024 kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 31 Disemba, 2023

No comments:

Post a Comment