Saturday, August 12, 2023

WAKURUGENZI MSIWAACHIE WALIMU KUSIMAMIA MIRADI PEKEE YAO - RC SERUKAMBA

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amewagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya mkoani hapa  kutowaachia walimu kwa asilimia 100 bila kufanya ufuatiliaji  suala la ununuzi wa vifaa vya ujenzi kwa ajili ya miradi ya shule inayotekelezwa kwa kuwa baadhi yao wameonekana kutokuwa na haraka kuikamilisha.

Ametoa agizo hilo jana Agosti 11, 2023 baada ya  kutembelea na kukagua ujenzi wa mabweni, madarasa na vyoo katika shule za Sekondari za kidato cha Tano za Ikungi, Ndago, Mwanamwema Shein, Lulumba na Tumaini zilizopo katika Halmashauri za Wilaya Iramba, Ikungi na Singida DC.

Serukamba alisema baadhi ya walimu ambao ndio wanasimamia ujenzi wa shule hizo wameonekana kutokuwa na uharaka kuijengea ikamilike kwa kuwa wameachiwa jukumu la kusimamia kwa asilimia 100 bila kufuatiliwa.

Akiwa katika shule ya Sekondari Ndago ambayo kasi ya ujenzi wa mabweni ni ndogo sana, alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba na Mhandisi kuanzia jana (Jumamosi) waanze kufika kila siku kwenye shule hiyo kufuatilia maendeleo ya ujenzi ili yakamilike kabla ya Ijumaa ya wiki iliyopita.

Aliwataka Wakandarasi ambao wamepewa zabuni za ujenzi wa shule hizo kuongeza idadi ya mafundi ili kasi ya kujenga madarasa na mabweni hayo iwe kubwa na kuanzia wiki ijayo yawe yamekamilika na kukabidhiwa kwa Serikali.

Mkuu wa Mkoa akiwa katika shule ya Sekondari Ikungi alitoa siku tatu kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kuweka vigae (tailizi) katika mabweni ya shule hiyo na Jumatatu apewe taarifa kuwa kazi hiyo imekamilika.

Serukamba alitoa agizo baada ya kukuta mabweni na madarasa ambayo Serikali ilitoa Sh. Milioni 811.7 yamewekwa sakafu ya saruji badala ya tailizi.

"Haiwezekani Serikali imetoa fedha za ujenzi zikiwamo za kuweka tailizi sakafu lakini mmeweka sakafu ya saruji, nawaagiza wekeni tailizi Jumapili jioni nitakuja kukagua ili Jumatatu nikabidhiwe mabweni rasmi,"alisema.

Serukamba akiwa katika shule ya Sekondari ya Mwanamwema Shein iliyopo Halmashauri ya Singida DC alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ester Chaula, kuongeza mafundi katika ujenzi wa mabweni ili kazi ikamilike haraka.

Aidha, aliwapongeza Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya kwa jinsi walivyosimamia miradi hiyo kwa ufanisi.




No comments:

Post a Comment