Tuesday, August 08, 2023

SINGIDA KUKABILIANA NA TATIZO LA MAFUTA YA KULA NCHINI

MKUU wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, amesema kuwa Singida imejikita katika kilimo cha alizeti ili kuhakikisha inazalisha kwa wingi mafuta ya kula yanayotokana na zao la alizeti kwa lengo la kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

Mkuu huyo ametoa maelezo hayo leo (tarehe 8 Agosti, 2023) wakati wa kilele cha maadhimisho ya maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Uvuvi yaliyohitimishwa Kanda ya Kati katika viwanja vya Nzuguni Jinini Dodoma.

Amesema kuwa Mkoa wa Singida umejipanga katika kilimo cha mazao ya kimkakati ikiwemo kilimo cha zao hilo lengo kubwa likiwa ni kuhakikisha Mkoa huo unakuwa na mafuta ya kutosha kwa soko la ndani na nje hatua hiyo itakuwa imepunguza kwa kiasi kikubwa gharama ya uagizaji wa mafuta hayo kutoka nje ya nchi.

“Mkoa wa Singida unategemea kilimo kwa asilimia 80 na wakazi wake wamekuwa wakijikita zaidi katika kilimo na kwa maana hiyo tunahitaji kuwa na kilimo cha kimkakati ambacho kitaweza kuwainuwa wakulima kiuchumi kwa kuwaongezea kipato wao wenyewe na taifa kwa ujumla” ameeleza Mkuu huyo wa Mkoa.

Aidha amesema kuwa Singida na Dodoma wamejipanga kufanya kilimo chenye tija ambacho kitaifanya mikoa ya Singida na Dodoma kuwa kitovu cha chakula nchini kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji katika skimu ya umwagiliaji zilizopo jambo ambalo litanyanyua uchumi wa Mkulima mmoja moja na taifa kwa ujumla wake.

Hata hivyo Serukamba amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassani kwa kuwekeza nguvu nyingi kwenye kilimo kwa maana ya kutoa pesa nyingi ambazo zitasaidia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji pamoja na kuwekeza katika uboreshaji wa pembejeo za kilimo, mifugo kwa njia ya uboreshaji wa majosho.

Amesema kitendo cha Rais Dk. Samia kuwekeza katika kilimo kitasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kusababisha kuwepo kwa mtawanyiko wa mvua ambazo hazieleweki.

“Kutokana na juhudi kubwa za Rais wa awamu ya sita kwa kuona umuhimu wa kuwekeza pesa nyingi kwenye kilimo, Serikali ya Singida kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imejipanga kuhakikisha inalima kilimo chenye tija na siyo kilimo cha kujikimu”

“Hata hivyo niwashauri Mabalozi kuhakikisha wanahamasisha kwa kuwatafuta wawekezaji wakubwa kuja nchini na kujenga viwanda vikubwa vya alizeti kwa ajili ya kuongeza mnyororo wa thamani na kwa kufanya hivyo vitajengwa viwanda vingi vya kuzalisha mafuta hayo na kusababisha uwepo wa mafuta ya kutosha”amesema Serukamba.

Sambamba na hayo amewapongeza washiriki wa makongamano ya maadhimisho ya kilimo, ufugaji na uvuvi kwa kushiriki semina na mafunzo mbalimbali ya kilimo cha Alizeti, Mtama na ufugaji wa Kuku pamoja na kutembelea mabanda mbalimbali kwa ajili ya kujifunza kilimo chenye tija na chenye kuwaletea manufaa.


No comments:

Post a Comment