Tuesday, July 18, 2023

RC SERUKAMBA ASISITIZA MIRADI YA BOOST MWISHO KUKAMILIKA IWE JUMAMOSI WIKI HII

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amefanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi shule mpya za msingi zinazojengwa kwa fedha za BOOST na kuagiza viongozi wa Halmashauri zote za Wilaya Mkoani hapa kuhakikisha ujenzi uwe umekamilika na shule hizo zikabidhiwe kwake ifikapo Jumamosi ya wiki hii.

 Serukamba ameyasema hayo leo (Julai 18, 2023) baada ya kutembelea miradi ya Boost katika Halmashauri za Wilaya ya Iramba, Mkalama, Singida Vijijini na Halmashauri ya Manispaa ya Singida.

 Katika Halmashauri ya Wilaya Iramba alitembelea na kukagua ujenzi wa shule mpya za msingi za Ng'anguli, Ishanga, Halmashauri ya Mkalama alitembelea shule mpya ya msingi ya Nkindiko na Shule ya Sekondari ya Tumaini.

“Tuligawana mimi na RAS, yeye alikwenda Wilaya ya Ikungi na Manyoni kuangalia na kukagua miradi ya boost ili kujionea hatua ya utekelezaji, kwakweli kazi kubwa imefanyika na nzuri, majengo yamejengwa kwa viwango” Serukamba

 Mkuu wa Mkoa wa Singida akiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida alitembelea na kukagua shule za Murya na Minyaa wakati katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida alitembelea shule mpya ya msingi ya Imbele na shule ya msingi Nyerere.

 Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara hiyo, Serukamba aliwapongezi viongozi wa Wilaya zote za Mkoa wa Singida kwa kusimamia vizuri miradi hiyo ambayo mingi imekamilika kwa asilimia 100 na michache ipo kati ya asilimia 90 na 95.

 "Nichukue nafasi hii kuwapongeza watendaji wenzangu kwa kweli miradi hii imekwenda vizuri, majukumu yetu tuendelee kuyafanya na niwaombe Madiwani na Wenyeviti wa vijiji wahamisishe wananchi kwa ajili ya kufanya usafi katika shule zilizojengwa ikiwa ni pamoja na kupanda miti kuzunguka shule," alisema Serukamba.

 Alisema katika kuhakikisha zoezi la upandaji miti linafanikiwa, wanafunzi wapewe miti ya kupanda na kuisimamia jambo ambalo litazifanya shule hizo kupendeza na kuwa na mazingira mazuri.

 "Tunapanga wiki ijayo tutakutana pale shule ya msingi Minga kwa ajili ya kufanya sherehe kubwa ya kupokea mradi huu ambao Mkoa wetu umepokea zaidi ya shilingi bilioni Tisa na tuishukuru sana Serikali ya awamu ya Sita," alisema.

 Serukamba alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejipambanua kwa kufanya kazi kubwa sana ya kuendeleza maisha ya watu kuwekeza kwenye maisha ya watu na vitu vinavyohusu watu.

 "Kuwekeza kwenye elimu ni kuwekeza kwenye mtu mmoja mmoja, ukiwekeza kwenye afya umewekeza kwenye afya ya mtu mmoja kimsingi Mhe. Rais amefanya kazi kubwa sana sana, pia hajaacha sekta za uchumi kama umeme, barabara kuna kazi kubwa sana imefanyika," alisema Serukamba.

 Ameongeza kuwa katika sekta ya umeme Mkoa wa Singida una vijiji 441 itakapofika Juni 2024 kila Kijiji kitakuwa kimepata huduma ya umeme na kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri alizofanya kwa Mkoa wa Singida.

MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA ZIARA HIYO.
















No comments:

Post a Comment