Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri wametakiwa kutumia kipindi cha siku thelathini (mwezi mmoja) kufanya utambuzi na uwekaji wa alama ya mipaka katika misitu iliyopo maeneo yao ikiwa ni pamoja na kutambua wamiliki wake ili ijulikane ukubwa wa msitu hiyo kwa ajili ya kuanza hatua za awali za kufanya biashara ya hewa ukaa.
Akiongea katika kikao kazi kilichofanyika tarehe 12 Mei,
2023 kilichotumika kutoa elimu ya Biashara ya hewa ukaa kilichofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt.
Fatma Mganga amesema Biashara hiyo itawaletea wananchi wa Singida utajiri
kupitia Misitu hiyo kama inavyofanyika katika maeneo mengine Duniani.
Aidha Dkt. Fatma alisistiza kutolewa elimu kwa wananchi kuhusu
utunzaji wa misitu na biashara hiyo ili wawe tayari kuilinda na kuongeza upandaji
wa miti sehemu ambazo hazina miti.
"Nashukuru tupo
na wenyeviti wa Halmashauri hapa najua litawafikia Madiwani, wataalamu wetu
tumieni vikao vya Madiwani kuwapa elimu na mhakikishe inawafikia wananchi"
Dkt. Mganga.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Pasikas Muragili
amesema tayari wana mtaji kwa kuwa wanamsitu wa Mgori Msikii na maeneo mengi
walishapanga matumizi bora ya ardhi.
Hata hivyo alibainisha kwamba wanaenda kukutana na wakala wa
misitu TFS ambao walishawakabidhi moja ya msitu wao ili waone namna
watakavyoshirikiana katika kulinda na kuhifadhi msitu ambao waliwakabidhi hivi
karibuni.
Awali akitoa elimu ya biashara ya ukaa muwezeshaji kutoka
Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika alisema Tanzania ina fursa kubwa kwakuwa
bado haijaathiri kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo alieleza kikao hicho kwamba yupo tayari kuja Mkoani Singida kushirikiana na wataalamu wa Mkoa huo katika kuandika mradi kuhusu biashara hiyo.
No comments:
Post a Comment