Tuesday, May 16, 2023

Dkt. Mganga ataka uwajibikaji katika kuinua ufaulu katika shule za msingi mkoani Singida

Maafisa Elimu  wote na Wakuu wa shule mkoani Singida wametakiwa kutumia mbinu mbalimbali kusimamia taaluma ili  kuhakikisha ufaulu unaongezeka katika shule za msingi.

Maelekezo hayo yametolewa leo na Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga wakati alipokutana na Wakuu wa shule na Maafisa elimu Mkoa, Maafisa elimu Wilaya, Maafisa elimu kata Mkutano uliofanyika Katika ukumbi wa mikutano ulipo katika shule ya Sekondari St. Bernard.

Akiwa katika kikao hicho RAS amewataka  Maafisa elimu kuwa watatuzi wa changamoto za Walimu ikiwa ni pamoja na kuzitembelea shule na kuja na mikakati ya kuboresha elimu kwa kuhakikisha kila mwalimu anatimiza majukumu yake na kufanya kazi kwa ushindani.

 Ameagiza wakuu wa shule kuwa na kawaida ya kufanya tathimini ya  kila wiki kwa walimu na masomo wanayo yafundisha ili kubaini mapungufu na namna ya kutatua  ambapo amesema itasaidia kuwapima kutokana na matokeo.

Dkt. Mganga amesema ni wakati sasa walimu hao pamoja na watendaji wengine wakiwemo maafisa elimu kutoka maofisi kwenda kwenye shule ambazo zinachangamoto ili kuinua hali ya elimu kwa kufanya tathmini ya wanafunzi ambao wanashindwa kuwa na matokeo mazuri.

“Twendeni tukafanye kazi, tuache ubosi, twendeni tukafanye tathmini tujue mwanafunzi gani anachangamoto ipi ili tuweze kuzikabili changamoto ambazo zinaturudisha nyuma kiwango cha elimu kwenye mkoa wetu”. Alisema Dkt. Mganga

“Kiongozi unaweka mikakati ili kuweza kupata matokeo usisikilize Rumors tumia jitihada zako upate matokeo ili uweke Legacy”. Aliongeza Katibu Tawala huyo.

Dkt. Mganga aliongeza kwa kusema kuwa viongozi wa Mkoa wa Singida wanapaswa kufanya kazi kwa kujituma ili waweze kuweka alama hivyo akasisitiza walimu wakuu kujituma na kujitoa zaidi kwenye kutoa elimu kwa wanafunzi.

Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Bahi, Boniface Willson ambaye alikuja kuwajengea uwezo walimu wa mkoa wa Singida alisema kuwa mwaka 2017 Halmashauri ya Bahi ilikuwa na shule ambazo zilikuwa hazifanyi vizuri kwenye elimu msingi hadi ikapewa bendera nyeusi lakini baada ya kufanya tathimini kwa sasa imekuwa ikifanya vizuri.

Willson alisema kujituma kwa walimu wakuu kwenye halmashauri hiyo ndiko kumeweza kubadilisha kutoka ufaulu wa chini na sasa imekuwa moja ya Halmashauri inayofanya vizuri ndani ki mkoa hadi kitaifa.


Naye Mratibu wa Programu ya Serikali ya Shule Bora Mkoa wa Singida Samweli Daniel amewashauri wadau wa elimu wanapopanga mipango ya kuboresha elimu iwe inaandikiwa ripoti ili zitumike wakati wa utekelezaji katika maeneo mbalimbali.


No comments:

Post a Comment