Mkoa wa Singida umeweka mikakati ya kuboresha elimu ya Sekondari ili kuhakikisha kwamba wanafuta daraja la mwisho (division zero) kuanzia mwaka huu 2022.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba wakati
akihitimisha Mkutano wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) uliofanyika katika
ukumbi wa mikutano Chuo cha Uhasibu Mkoani hapo.
Amesema Serikali ya Mkoa imedhamiria kuinua kiwango cha elimu
kwa kuhakikisha wanaanza kufuta daraja sifuri na hatimaye watafikia daraja la
tatu.
Amesema ili kufanikiwa katika zoezi hilo ni lazima wazazi,
walimu, wanafunzi na viongozi wa Dini na jamii kwa ujumla washirikiane na viongozi
wa Serikali kuandaa na kutekeleza mkakati huo ili ulete matunda.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Mwl. Dororthy
Mwaluko amesema tayari ameshafanya kikao na Walimu wakuu wote na Maafisa elimu
kata ambapo waliandaa viwango vya kuwapima kwa kila kata na kila kila shule.
Aidha amesema jumla ya shule za Sekondari 146 kati ya shule
168 za Serikali zimeandaliwa kutoa chakula cha mchana ili kuwavutia wanafunzi
kuja shule na kupata nguvu ya kusoma.
RAS ameendelea kusema kwamba mpango huo utaendelea
kutekelezwa katika shule za Sekondari huku akibainisha kwamba kwa upande wa
shule za msingi bado zoezi halijakaa sawa ambapo jumla ya shule 187 kati ya
shule 609 ndizo zinazopata chakula.
Hata hivyo Mwaluko ameeleza kwamba jitihada nyengine
walizofanya ni kuteua Wakuu wa shule katika shule mpya zilizojengwa na kufanya
uhamisho wa walimu waliopo ili kukidhi haja ya upungufu wa walimu.
Akimalizia hotuba yake Mwaluko ameeleza kwamba Mkoa wa Singida umeanzisha mpango ujulikanao "Singida Digital Class" ambapo wanafunzi hutumia video za masomo yaliyorekodiwa ili kujifunzia hasa katika shule ambazo hazina walimu wa masomo husika.
No comments:
Post a Comment