Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amesema wapo katika mchakato wa kutangaza tenda katika maeneo ya minada na masoko kwa kuwa kwa sasa makusanyo ya mapato yanayopatikana katika maeneo hayo ni kidogo ikilinganishwa na uhalisia.
RC Serukamba ameyasema hayo leo wakati akiendesha kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Uhasibu mjini hapa ambapo alieleza upotevu wa fedha kupotea katika maeneo hayo.
Amesema amegundua kwamba katika masoko yaliyopo katika Manispaa ya Singida vipo vibanda ambavyo vinalipa shilingi Laki moja na nusu huku vya kwao vikiwa vinalipa Laki moja tu.
"Yapo mabanda wanalipa laki mbili na nusu lakini ya kwetu tunalipwa laki moja na nusu, hii haiwezekani tutafute mtu atukusanyie shilingi laki mbili kwa mwezi na inawezekana" alisema Serukamba.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Singida wakifuatilia agenda mbalimbali wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa huo Novemba 16, 2022
Aidha ameendelea kuwakumbusha Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo kuhakikisha wanafuatilia waliokusanya mapato na kutoyapeleka benki na kuhakikisha wanafanya hivyo.
Fedha ambazo bado zipo mikononi mwa wakusanya ushuru kwa Halmashauri zote za Mkoa wa Singida ni zaidi ya Bilioni 1 ambazo zingeweza kusaidia kumalizia miradi mbalimbali iliyobaki aliendelea kusema Rc Serukamba.
No comments:
Post a Comment