Tuesday, October 18, 2022

RC Serukamba akutana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba leo amekutana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi Neema Mwakalyelye na kujadili mambo kadhaa kuhusiana na kuzuia vitendo mbalimbali vya rushwa katika miradi na shughuli mbalimbali za kijamii.

Akiwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi huyo amesema lengo la ziara yake ni kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanyika Mkoani hapo ikiwa ni Mkakati mojawapo wa TAKUKURU kupinga na kupambana na rushwa.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi Neema Mwakalyelye akizungumza wakati wa kikao na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba

'Ki msingi hapa tunatekeleza agizo la Rais linalotutaka tujikite zaidi katika kuzuia upotevu na ufujaji kabla fedha haijapote, kama tukiweza kuepuka hayo tija itakuwa kubwa." Amesema Mwakalyelye

Hata hivyo Mkurugenzi huyo amesema katika ziara yake anategemea kufanya kikao kazi ambapo atakutana na Watumishi wake kwa lengo la kutoa mafunzo kazi pamoja na kamati za maadili zilizopo Mkoani hapo.

Aidha amesema TAKUKURU imeendelea kujikita katika uzuiaji wa rushwa za aina zote kwa lengo la kuondoa ubazilifu na upotevu wa fedha za Serikali, ambapo amebainisha kuwa kwakufanya hivyo tija itakuwa kubwa na Watanzania watafaidi matunda ya nchi yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amepongeza ziara ya Mkurugenzi huyo huku akibainisha kwamba itasaidia katika kuzuia vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikiendelea katika minada na miradi mbalimbali Mkoani hapo.

Amesema rushwa ikidhibitiwa kikamilifu Serikali itaokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kimekuwa kikikpotea au kuliwa na watu wachache na hata kiwango cha makusanyo ya mapato kitaongezeka.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akizungumza katika kikao wakati alipotembelewa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi Neema Mwakalyelye

" Binafsi nipongeze ziara yako kwa kuwa naamini itasaidia kuziba mianya ya rushwa, ninaamini ukipita huko kwenye miradi wataamini tunafatiliwa wataacha vitendo vya rushwa" alisema Serukamba

RC Serukamba ameeleza kwamba kwa ushirikiano baina ya Mkoa na TAKUKURU kutasaidia kubuni mipango Mkakati wa kufuatilia hasa katika miradi ya maendeleo na minada tutapunguza rushwa kwa kiasi kikubwa.


Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi Neema Mwakalyelye akielezea lengo la ziara yake mkoani Singida wakati alipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Singida ofisi kwake.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akielezea jambo katika kikao, wakati alipotembelewa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi Neema Mwakalyelye.



Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akipoea vitabu mbalimbali vinavyoelezea kuhusu TAKUKURU pamoja na mwamvuli wemye nembo ya TAKUKURU kutoka kwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi Neema Mwakalyelye.

Kikao kikiendelea ofisi kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (wa nne kutoka kushoto), Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi Neema Mwakalyelye (wa nne kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Singida wakati wa ziara hiyo.

No comments:

Post a Comment