Thursday, October 13, 2022

RC Serukamba aagiza Vyama vya Ushirika viimarishwe ili kujenga uchumi wa Mkoa

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ameagiza kuanzishwa na kuimarishwa vyama vya Ushirika  Mkoani hapo  ili viweze kutoa huduma kwa wananchi na kutatua changamoto za soko pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma mbalimbali katika maeneo husika.

Rai hiyo ameitoa leo 13 Octoba, 2022 akiongea na wanaushirika katika jukwaa la Maendeleo ya Ushirika lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Uhasibu Mkoani hapo.

RC Serukamba ameeleza kwamba  Sekta za kipaumbele na kiuchumi katika Mkoa wa Singida ni kilimo, madini na ufugaji na vyanzo vikuu vya mapato katika Mkoa wetu. Hivyo ni muhimu kuvitambua vipaumbele katika kuanzisha na kuimarisha Vyama vya Ushirika katika sekta ya kilimo, ufugaji na madini ili viweze kutoa huduma kwa wananchi kama inavyotarajiwa.

"Ninawaelekeza Wakurugenzi wote kwa kushirikiana na Mrajishi wa Vyama vya Ushirika na Maafisa Ushirika katika Halmashauri kuweka mpango katika kila Halmshauri kuanzisha Vyama vya Ushirika vya aina mbalimbali kwa kuanzia na mazao ya kimkakati Korosho, Mkonge, Tumbaku na Alizeti, sambamba na kuimarisha vyama vya Ushirika vilivyopo katika maeneo yenu". Alisema Serukamba.

Serukamba alibainisha kwamba Serikali inahimiza uanzishwaji wa Vyama imara katika sekta mbalimbali za kiuchumi vinavyotoa matarajio ya wanachama ikiwa kama nyenzo muhimu ya Maendeleo.

Aidha, Vyama vya Ushirika vinapaswa vitumike kuchochea kasi ya Maendeleo ya Taifa na hivyo kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi katika Mkoa wa Singida.

Hata hivyo amewataka Viongozi na Watendaji wote wa Vyama vya Ushirika kusimamia na kuendesha vyama hivyo kwa kuzingatia sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013, Sheria ya huduma ndogo za Kifedha ya mwaka 2018 na kanuni zake wakati wote wa uendeshaji wa vyama vya Ushirika na kujiepusha na ubadhirifu, wizi, matumizi mabaya ya madaraka, kutokuwajibika na uzembe kwa kuwa vitendo hivyo vinasababisha Vyama vya Ushirika kuendelea kuzorota na kushindwa kutoa huduma kama ilivyotarajiwa.

Serikali ya awamu ya sita haitawavumilia kamwe viongozi na watendaji wa Vyama vya Ushirika watakaofanya ubadhirifu, wizi na kusababisha hasara katika Vyama vya Ushirika  na kwamba yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kuondolewa madarakani, kufikishwa Mahakamani na kufidia hasara zote zitakazojitokeza.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA











No comments:

Post a Comment