Wednesday, September 28, 2022

RC Serukamba amaliza Mgogoro wa mashamba ya Mpambaa na Kinampundu Mkoani Singida uliodumu kwa miaka zaidi ya miwili.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba leo tarahe 28.09.2022 amemaliza mgogoro wa shamba la mbegu lililopo Kata ya Mpambaa Wilaya ya Singida Vijijini na Kinampundu Wilaya ya Mkalama lenye  ukubwa wa ekari 456.82 uliodumu kwa miaka zaidi ya miwili.

Akiongea katika mkutano wa hadhara uliowahusisha wananchi wa kata hizo mbili Mkuu wa Mkoa amesema shamba hilo litagawanywa katika sehemu mbili ambazo ni  ekari 222.5 zitakazo milikiwa na  Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na ekari 234.32 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Vijijini kwa kuzingatia mipaka iliyoainishwa kisheria kwenye G.N.

“Timu ya Wataalam iliyoundwa ilipitia mipaka ya kisheria kwa mujibu wa G.N. Na. 160 ya tarehe 15 Novemba, 1935, GN Na. 287 ya 9 Septemba, 2011 zinazohusu Halmashauri ya Wilaya ya Singida na Tangazo la uanzishaji Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama la 26 Juni, 2013”. Alisema

Aidha, Rc Serukamba amesema kwamba Halmashauri zote mbili ziyapime mashamba hayo yaliyogawanywa na kuyasimamia uendeshaji wake ili wananchi wa Vijiji husika wanufaike kwa kuendeleza kilimo, ufugaji na shughuli nyinginezo za uzalishaji mali.

Rc Serukamba akabainisha kwamba Vijiji vilivyopo eneo la mashamba hayo vipewe kipaumbele cha kuandaliwa mipango ya matumizi Bora ya ardhi ili kuepuka migogoro mingine ndani ya maeneo ya Utawala wa Vijiji.

Hata hivyo Serukamba akaagiza kuwekwa alama za mipaka (Beacon) maeneo ya mita 100 mpaka 200 kwenye maeneo ya mpaka na wananchi wapewe elimu ili kuepuka migogoro kama hiyo kutokea tena.

Mkuu wa Mkoa huo ameziagiza Halmashauri hizo pamoja na Serikali za Vijiji katika mashamba hayo zihakikishe wananchi watakaopewa maeneo ya mashamba hayo wahakikishe wanayalima ili yasiwe Mashamba pori huku akisistiza mgao huo uwalenge zaidi vijana na wanawake ili kupunguza tatizo la ajira.

Awali Mkuu wa Mkoa alisema kwamba Shamba la mbegu la Mpambaa lililokuwa linamilikiwa na Mkoa wa Singida, ambalo limekuwa likutumika kwa shughuli za Kilimo. Aidha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilipokea malalamiko kuhusu umiliki halali wa shamba hilo mwezi Februari, 2022 kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida au Mkalama.

Katika kutatua, sintofahamu hiyo, Mkoa uliunda timu ya Wataalam iliyopewa hadidu za rejea zilizojumuisha kubaini eneo la shamba, kubaini liko katika mamlaka ya Halmashauri gani na uendeshaji wake.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akizungumza na wananchi waliojitokeza kushuhudia tamko la Serikali kuhusu mgogoro wa shamba kati ya Singida Dc na Mkalama Dc.





Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kushoto) akiongoza timu ya wataalamu na wajumbe mbalimbali waliojitokeza kushuhudia suruhisho la mgogoro wa shamba kati ya Singida Dc na Mkalama Dc ili kutatua mgogoro wa shamba.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akiwa katika eneo linalogawa pande mbili za shamba akionyesha mipaka iliyoonyeshwa kwenye ramani inayoonyesha mipaka kati ya Singida Dc na Mkalama Dc ili kutatua mgogoro wa shamba.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisoma ramani inayoonyesha mipaka kati ya Singida Dc na Mkalama Dc ili kutatua mgogoro wa shamba.

Mkuu wa Wilaya ya Singida Vijijini Paskas Muragili akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida ili kutatua mgogoro wa shamba.

Mkutano wa ukiendelea

No comments:

Post a Comment