Wednesday, September 21, 2022

MKUU WA MKOA WA SINGIDA AWAASA VIJANA WALIOJIUNGA NA JKT KUZINGATIA NIDHAMU NA UZALENDO

 

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amewaasa vijana waliochaguliwa kwenda kujiunga na Jeshi  la Kujenga Taifa (JKT) mkoani hapa kuzingatia nidhamu na uzalendo katika kipindi chote watakapokuwa kwenye mafunzo.

Ametoa rai hiyo wakati akizungumza na vijana takribani 306 wakati akiwaaga rasmi baada ya zoezi la usahili, upimaji na uandikishaji kumalizika ambapo amesisitiza kwamba vijana hao wataanza kuondoka Septemba 27, mwaka huu kwenda kwenye kambi mbalimbali walizopangiwa kwa ajili ya kuanza mafunzo.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko, akizungumza na vijana hao.

Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko, alisema nidhamu na uzalendo wa kuipenda nchi vipewe kipaumbele wakati wa mafunzo hayo ambayo yatachukua miaka miwili.

"Utovu wa nidhamu umejaa kila kona sasa nendeni mkijua sisi ni Watanzania sasa vile vitabia vyenu vyote vya kijinga wekeni pembeni wewe ni kwenda kufuata amri tu," alisisitiza Mwaluko.

Alisema ikiwa vijana hao watatuliza vichwa vyao wajiwa kwenye mafunzo, sanjari na maelekezo watakayopewa huko jeshini ni dhahiri baada ya kupata mafunzo hayo na kurejea uraiani watakuwa tofauti na raia wengine.

Mshauri wa Jeshi la Akiba Mkoa wa Singida Kanali Rhinoceros Magemeson akizungumza na vijana hao.

Awali akitoa taarifa ya mwenendo wa zoezi la mchakato huo, Mshauri wa Jeshi la Akiba Mkoa wa Singida Kanali Rhinoceros Magemeson, amesema vijana hao wamepatikana baada ya kufanyiwa usaili na vipimo vya afya zoezi lililosimamiwa na viongozi kutoka makao makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa lililoongozwa na Meja Bituro Magere Maingu (Mkuu wa Msafara wa Upimaji Afya) ambalo lililoanza Septemba 14 hadi 21 mwezi huu.

Kambi ambazo watakwenda kujiunga ni 824KJ Kanembwa iliyopo Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, 825KJ Mtabila iliyopo Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, 821KJ Bulombola mkoani Kigoma, 826KJ iliyopo Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, 822KJ Rwamko iliyopo Wilaya ya Musoma mkoani Mara na 823KJ Msange iliyopo mkoani Tabora. 


Baadhi ya vijana waliochaguliwa kwenda kujiunga na Jeshi  la Kujenga Taifa (JKT) kutoka mkoani Singida. 
 Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko (kushoto) akisalimiana na baadhi ya viongozi kutoka makao makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa lililoongozwa na Meja Bituro Magere Maingu (Mkuu wa Msafara wa Upimaji Afya) ambalo lililoanza Septemba 14 hadi 21 mwezi huu mkoani hapa.

No comments:

Post a Comment