MAAFISA Afya mkoani Singida
wameagizwa kuzitumia sheria zilizopo kwa kuwachukulia hatua baadhi ya watu
wanaochafua mazingira maeneo mbalimbali ya mijini na vijijini yakiwamo ya
barabara kuu na kwenye makaburi.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida,
Dorothy Mwaluko, ametoa agizo hilo leo tarehe 16 Septemba, 2022 wakati wa kikao
kazi cha Maafisa Afya kutoka halmashauri za mkoani hapa katika hotuba
iliyosomwa kwa niaba yake na Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO), Dk. Victorina Ludovick.
Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO), Dk. Victorina Ludovick akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho.
Alisema Serikali ya awamu ya sita
inathamini sana suala la usafi wa mazingira kwani ndio mhimili mkubwa wa Afya
ya Watanzania na ukuaji wa uchumi.
"Tumieni sheria ya Afya ya Jamii
ya mwaka 2009 na kanuni zake, sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004
pamoja na sheria ndogo za miji kuhakikisha maeneo ndani ya Mkoa wa Singida
hayachafuliwi hovyo ikiwemo barabara kuu, stendi, masoko, mitaro, maeneo ya
wazi, makazi na makaburi," alisema.
Mwaluko alisema maeneo ya masoko na
biashara wananchi waweke vyombo vya
kuhifadhia taka vyenye ukubwa wa kutosha kulingana na uzalishaji wa taka kwa
lengo la kupunguza taka kuzagaa ovyo mitaani.
Alisema yapo baadhi ya magari ya
abiria yanasimama maporini na abiria kuchimba dawa (kujisaidia) vichakani jambo
ambalo halikubariki hivyo Maafisa Afya wahakikishe wanachukua hatua.
Mwaluko alisema Maafisa Afya wa
Mkoa wa Singida wanafanya kazi vizuri kutekeleza kampeni ya Taifa ya Usafi wa
Mazingira lakini lazima kuhakikisha fedha inayotolewa na Serikali matokeo yake
yanaonekana.
Aliongeza kuwa Wakurugenzi wa
Halmashauri, Waganga Wakuu, Maafisa Afya na Watendaji wa vijiji na kata
wasimamie ili kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo bora.
Alisema taarifa zilizopo hadi 31
Julai, 2022 kaya zenye vyoo katika Mkoa wa Singida ni asilimia 99.2 na
zisizokuwa na vyoo ni asilimia 0.8, zenye vyoo bora ni asilimia 62.1 kutoka
asilimia 27.6 mwaka 2015.
"Mimi kama Katibu Tawala wa
Mkoa wa Singida, sitavumilia kuona magonjwa ya aibu kama vile kipindupindu
yakitokea katika mkoa wangu hivyo mjipange katika hili," alisema Mwaluko.
Aidha, alisema Maafisa Afya
watambue kuwa wao kama wasimamizi na
wafuatiliaji Wakuu wa shughuli za chanjo, ukaguzi wa dawa, ukaguzi wa vyakula
na ukaguzi wa vituo vya kutolea huduma za Afya mashuleni na taasisi zote
waongeze bidii kusimamia hayo.
Afisa Afya Mkoa wa Singida, Mgeta Sebastian akizungumzia hali ya mazingira kwa mkoa huo.
Naye Afisa Afya Mkoa wa Singida,
Mgeta Sebastian amesema kwamba wakati sasa umefika kwa Maafisa Afya kuhakikisha
wanasimamia ili kuweka mazingira safi maeneo yote ya mkoa huo.
Sebastian amesisitiza kuwa katika
suala la usimamizi wa afya atakuwa mkali na kwamba afisa afya asiyetekeleza majukumu
yake kama inavyotakiwa atachukuliwa hatua ikiwamo kumripo kwa wakuu wake.
MATUKIO KATIKA PICHA
No comments:
Post a Comment