Saturday, August 27, 2022

WASIMAMIZI WA SENSA SINGIDA WATAKIWA KUWAFUATILIA MAKARANI KUZIFIKIA KAYA AMBAZO HAZIJAHESABIWA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amewataka Wasimamizi wa Makarani wa Sensa waliomaliza kufanya madodoso katika maeneo waliyopangiwa kuwahamisha kwenda kuongeza nguvu maeneo mengine ambayo bado zoezi la Sense halijawafikia wananchi.


RC Serukamba amesema hayo baada ya kukagua zoezi la Sensa kwenye Kaya za Singida Mjini, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na Itigi Mkoani humo ambapo amesisitiza Kamati za Sensa za kila Halmashauri kuongeza kasi ya kuzifikia Kaya hadi kufikia Jumatatu ya Agosti 29 ili kufanikisha zoezi hili.


“Zoezi linaenda vizuri sana, na utaona tumeshaandikisha watu wengi sana Halmashauri zingine zimefikia asilimia 80% ukiacha halmashauri ya itigi ambayo inachangamoto ya geografia yao ya umbali hivyo kuwalazimu Makarani kutembea umbali mrefu lakini tumeweza kuwajazia mafuta kwenye pikipiki ili wazifikie Kaya nyingi”. Alisema RC Serukamba.


Ameongeza kuwa ili kuongeza kasi hiyo ya kuandikisha Kaya nyingi zaidi Wasimamizi wa Sensa pamoja na Waratibu wawe karibu kuwafuatilia Makarani ili watakapomaliza maeneo waliyopangiwa wahamishiwe kwenye Kaya zingine ambazo hazijafikiwa.


“Msisitizo wangu nimewambia ni kuwa wale Makarani waliomaliza zile kaya walizopangiwa wahamishiwe kwenye Kaya zingine nimewaambia maafisa takwimu wa wilaya kufanya hilo na tumeona kote nilikopita wapo Mkarani ambao wamemaliza Kaya walizopangiwa na wamepewa Kaya zingine nia yetu ni kutaka tusaidiane ili tuweze kumaliza vizuri”. Aliongeza RC Serukamba.


Naye Mratibu wa Sensa Mkoa wa Singida Naing’oya Kipuyo amesema kuwa kuletwa kwa vifaa vya kuchajia vishikwambi pamoja na kutumia bakaa ya fedha kwaajili ya kuwawekea Makarani mafuta ili kuzifikia Kaya zilizopo mbali imeongeza kasi ya uandikishaji wa Kaya ikilinganishwa na hapo awali ambapo Karani alikuwa analazimika kuacha zoezi hilo kutokana na umbali na vishikwambi kukosa chaji.


“Serikali imetoa ruhusa ya kutumia bakaa ya fedha kurahisisha zoezi hili Waratibu wa Sensa wa Wilaya ama kwenye Halmashauri wamekuwa wakikodisha jenereta na pikipiki na kuweka mafuta kuhakikisha zoezi linamalizika katika siku saba ambazo zimepangwa.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA



Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akimsikiliza Karani wa Sensa ya Watu na Makazi wakati wa ziara yake Singida Mjini leo tarehe 27 Agosti 2022.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisisitiza jambo kwa Kiongozi wa Makarani wa Sensa katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi wilayani Manyoni wakati wa ziara yake leo tarehe 27 Agosti 2022 mkoani humo.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akizungumza na Karani wa Sensa Wilayani Ikungi wakati wa ziara yake leo tarehe 27 Agosti 2022 mkoani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kulia) akiwa katika maeneo ya Singida Mjini kwa lengo la kutembelea kwenye Kaya kujionea hali ya utekelezaji ya zoezi la Sensa mkoani humo Agosti 27, 2022

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akizungumza na Waratibu wa Sensa ya Watu na Makazi katika Wilaya ya Ikungi (hawapo pichani) wakati wa ziara yake leo tarehe 27 Agosti 2022 mkoani humo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi akisoma taarifa ya utekelezaji wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa kipindi cha kuanzia tarehe 21 hadi 26 Agosti 2022 kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.


Mkuu wa Mkoa wa Singida akiongoza viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwenda kujionea utekelezaji wa zoezi la Sensa katika Wilaya hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisalimiana na moja ya Mkuu wa Kaya katika kijiji cha Ikungi  aliyeshiriki kuhesabiwa mara baada ya kutembelea kwenye Kaya kujionea hali ya utekelezaji ya zoezi la Sensa mkoani humo Agosti 27, 2022

No comments:

Post a Comment