MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amewataka Makarani na Wasimamizi wa SENSA mkoani hapa wasifanye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kama ni la kuja kutafuta posho tu.
Akizungumza na Makarani na Wasimamizi hao ambao wanaendelea
na mafunzo mjini Singida, alisema jukumu walilopewa ni kubwa sana linahitajika
kufanywa kwa umakini ili taifa lipate takwimu sahihi za watu kwa ajili ya
kupanga mipango ya maendeleo.
"Zoezi hili ni kubwa la kitaifa ambalo linahitaji
umakini wa hali ya juu na watakalofanya lifanikiwe ni nyie hivyo tusilifanye
zoezi la Sensa kama ni la kuja kutafuta posho, inawezekana wengine wapo hapa na
vishikwambi anayofundishwa haelewi kikubwa muhimu kwake apate hela jioni, utakuwa
hujaisaidia nchi yako," alisema.
Serukamba alisema kupitia Sensa hii nchi itaweza kujua idadi
ya maskini, watu wanahitaji shule, afya
na maji kiasi gani hivyo vijana watambue wameaminiwa na nchi waifanye
kazi ya Sensa kwa umakini sana.
Alisema mtihani kwa wasimamizi na makarani wa Sensa ni
kuifanya kazi kwa weledi na kuleta takwimu sahihi ambapo wakiifanya vizuri kazi
hii Serikali itakapokuwa na kazi nyingine wao ndo watapewa kipaumbele kupewa.
"Mkoa unawategemea sana kupata takwimu sahihi na
kuufanya uwe miongoni mwa mikoa itakayofanya vizuri katika zoezi hili la Sensa
ambalo hufanyika kila baada ya miaka 10," alisema.
Serukamba alisema makarani na wasimamizi watapewa madodoso
hivyo ni muhimu wajifunze mbinu za kuwauliza wananchi ili kuwafanya wawaelewe
watakapokuwa wakiwadadisi.
"Kuja mtu unaweza kumuuliza una ng'ombe wangapi
akashindwa kueleza pengine akidhani unataka kuja kunyang'anya ng'ombe wao
...hapana ni muhimu kujifunza mbinu za kumfanya mtu akuelewe sababu majibu
yenyewe yanatokana na maswali rahisi atakayoulizwa," alisema.
Aliongeza kwa mfano Tanzania inaelezwa ni nchi ya pili katika
Afrika kwa kuwa na mifugo mingi baada ya Ethiopia lakini ukiuliza tuna ng'ombe
au mbuzi wangapi hakuna anayejua.
Alisema Sensa inakwenda kuleta majawabu yote hayo
kinachohitajika ni umakini kwa makarani na wasimamizi wa Sensa ya Watu na
Makazi walioaminiwa na Serikali kuifanya kazi hiyo kwa umakini na weledi wa
hali ya juu.
Naye Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi Mkoa wa Singida, Mratibu
wa Sensa Mkoa wa Singida, Naing’oya Kipuyo, makarani 445 wamehitimu mafunzo yao
ya dodoso la Sensa ambalo watahoji majengo na makundi maalum.
Alisema kundi la pili ni la wasimamizi wa maudhui ambao
watahoji dodoso la jamii ambao wapo 212 ambao wataendelea na mafunzo kwa siku
tatu.
MWISHO
No comments:
Post a Comment