VIONGOZI wa Taasisi za Umma na binafsi mkoani Singida, wamehimizwa
kuhakikisha wanajenga mazingira rafiki baina yao na watumishi wanaowaongoza ili
kuongeza tija na uwezo wa kutoa huduma mbalimbali zitakazo kidhi mahitaji ya
wananchi.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy
Mwaluko wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa Wiki ya Utumishi wa Umma mkoani
Singida uliyofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa mkoa huo Juni
16, 2022.
Amefafanua kwamba wiki ya Utumishi wa umma inalenga kuhamasisha
na kuwakumbusha watumishi wa sekta ya umma na binafsi kujua wajibu wao katika
kuwahudumia wananchi pamoja na kutambua miiko mila na desturia za utumishi wa
umma ambazo zitasaidia kuongoza mahusiano mazuri katika kutekeleza majukumu ya kazi.
“Ili wananchi waweze kuhudumiwa
ipasavyo kiongozi wa Taasisi ni lazima awe na mahusiano mazuri na watumishi
anaowaongoza. Pia awe na utamaduni wa kuwatembelea watumishi wa chini yake na
kujua changamoto zinazowakabili. Changamoto ambazo zipo kwenye uwezo wao wazitatue
mapema iwezekanavyo”. Amesisitiza
Mwaluko.
Amewasisitiza kutoa huduma kwa wananchi bila upendeleo au
ubaguzi wowote na pale wanapokutana na changamoto ambazo zitakuwa juu ya uwezo
wao waziwakilishe kwenye mamlaka husika ili ziweze kutafutiwa majibu.
“Wapo baadhi ya viongozi wa taasisi za umma au binafsi hawapo
karibu na watumishi wa chini yao. Mtumishi akifanya kakosa kadogo kiongozi
badala ya kusaidia kutatua anatishwa na kuambiwa atachukulia hatua kali dhidi
ya mtumishi huyo. Tabia hii haijengi na haivumiliki kabisa”. amesema RAS
Mwaluko.
Mwaluko amesema ni kweli tunapashwa kusimamia sheria kanuni na
taratibu lakini wakati mwingine busara zinatakiwa zitumike hasa
ukizingatia binadamu ni mtu wa makosa.
Aidha, ameonya viongozi wengi wa taasisi za umma na binafsi
ambao hawajishughulishi na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi walio
chini yao kitendo hicho kinachochea watumishi hao kukimbilia ofisi ya Katibu
Tawala Mkoa ambayo imegeuka kuwa kama kliniki.
“Tarehe 23 mwezi wa Nane Sensa tujiandae kuhesabiwa
na tukawahimize wananchi wanaokuja kupata huduma kwetu ili waweze kutambua hiyo
tarehe kwa ajili ya SENSA ya mwaka huu”. Amesisitiza Dorothy Mwaluko
Kwa upande wake Katibu Chama cha Walimu Mkoa wa Singida, Mwalimu
Suzan Shesha ametumia nafasi hiyo kumshukru na kumpongeza Katibu Tawala Mkoa
huo Dorothy Mwaluko kwa kubuni na kuanzisha wiki ya utumishi wa umma ambayo
itasaidia katika kubadilishana uzoefu na kuongeza hali ya utendaji katika
kuwahudumia wananchi.
“Kukutanisha viongozi wa taasisi za umma na binafsi mama yetu
Dorothy Mwaluko ameona mbali sana. Sisi viongozi tumepata nafasi ya kutoa
changamoto zinazotukabili na zimepatiwa majibu wakati huo huo. Ili kumuunga mkono
Katibu Tawala wetu tunaenda kuhakikisha walimu wanawajibika ipasavyo”. Amesema Suzan
Shesha
Aidha, Suzan ametumia fursa hiyo kumshukru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa mambo mengi mazuri anayowatendea
watumishi wakiwemo walimu katika kutatua changamoto mbalimbali pamoja na
ile sugu ya kupandishwa madaraja.
Naye, Katibu Chama cha walimu Wilaya ya Mkalama, Amani Msange amesema yale yote aliyoagiza Katibu Tawala Mkoa wanaenda kuyafanyia kazi ikiwemo kutembelea watumishi na kujua changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu.
No comments:
Post a Comment