Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa huo Dkt Binilith Mahenge alipokutana na wawakilishi wa shirika la kimataifa la Chakula na Kilimo Duniani (WFP) pamoja na wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Maafisa kilimo katika ukumbi wa Mkoa huo ambapo alibainisha kwamba changamoto ya upatikanaji wa mbegu bora, masoko na upotevu mazao baada ya kuvunwa vitapatiwa ufumbuzi siku chache zijazo.
Amesema Shirika hilo limekuja na Mradi wa kuwasaidia wakulima wa Singida kuongeza uzalishaji wa alizeti, mtama na mazao ya bustani na vikolezo katika vijiji visivyopungua 50 na visivyozidi 70 huku akibainisha kwamba mradi huo umekuja na suluhisho la soko kwa mazao ya wakulima hao.
Aidha RC Mahenge amependekeza Mradi huo kushirikiana na Halmashauri kuzalisha mbegu za alizeti na mtama kwa kuwa Halmashauri zina uwezo na maeneo yenye kufaa uzalishaji huo.
Hata hivyo RC Mahenge akizitaja Taasisi ya Magereza kuwa mradi huo pia unaweza kushirikiana katika kuzalisha mbegu za alizeti na mtama kwakuwa wana maeneo na nguvu kazi ya kutosha ili kuondoa tatizo la upatikanaji wa mbegu Bora kwa wakulima wa Mkoa huo.
Awali akiutambulisha Mradi huo Mkuu wa Ofisi ya mahusiano Shirika la chakula duniani Neema Mina Sitta alisema Mradi una malengo ya kuongeza uzalishaji wa mtama alizeti pamoja na mboga mboga ili kuchangamkia fursa ya soko inayopatikana katika nchi ya Sudani pamoja na viwanda vya uzalishaji wa vinywaji hapa nchini.
Amesema Mradi utaongeza uzalishaji kwa kuboresha upatikanaji wa mbegu kutokana na ushirikiano baina yao na Shirika la utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) ambapo watazalisha mbegu mama.
Aidha Mradi huo utawaunganisha wakulima na masoko na utasaidia kuongeza thamani ya mazao ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vidogo vidogo katika maeneo ya uzalishaji alisema Neema.
Kwa upande wake Afisa Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na uzalishaji Beatusi Choaji ameeleza kwamba Mkoa una wakulima wachapakazi na kazi ya uzalishaji wa mbegu unaweza kufanywa na vikundi vya wakulima ambavyo tayari vilishaundwa hivyo kuomba zoezi hilo liwe endelevu ili kuwasaidia wakulima mkoani hapo.
Hata hivyo Mhandisi Paskasi Muragili akawaomba Shirika hilo kwamba Mradi huo ujikite katika kilimo cha umwagiliaji ili kuwa na kilimo cha uhakika na cha kibiashara. Huku alibainisha kwamba Wilaya ya Singida Vijijini ipo tayari kupokea mradi huo na itaendesha kikamilifu kilimo cha alizeti na Mtama.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Binilith Mahenge akizungumza wakati wa kikao hicho
No comments:
Post a Comment