Monday, April 11, 2022

Watoto 292,857 Kupata Chanjo Ya Polio Mkoani Singida

 

Mkoa wa Singida umedhamiria kutoa chanjo ya polio kwa jumla ya watoto  292,857 wa kuanzia umri wa Miezi 0 Hadi 59 ili kuzuia mlipuko wa Ugonjwa huo na kuongeza Kinga jamii  kwa watoto wote wa chini ya miaka mitano.

Akitoa wasilisho lake katika Kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuhusisha wajumbe mbalimbali kutoka Halmashauri Saba za Mkoa huo, wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na wadau mbalimbali Mratibu wa chanjo mkoani Singida Habibu Said Mwinory amesema chanjo hiyo itatolewa kuanzia tarehe 21- 24 Aprili  2022 katika maeneo yote ya mkoa huo ambapo Kampeni hiyo itakuwa ya nyumba kwa nyumba na mtoto kwa mtoto.

Aidha bwana Habibu amesema idadi hiyo ya watoto wanaotegemewa kupata chanjo watatoka Halmashauri Saba za mkoa huu zikuhusisha Wilaya za Mkalama, Iramba, Singida DC, Ikungi, Manyoni na Itigi ambapo jumla ya chanjo 336,800 zinategemewa kutumika katika maeneo hayo.

Hata hivyo Mratibu huyo  amebainisha lengo la programu hiyo ya  chanjo ni kuongeza uelewa wa kutosha kwa watoa huduma na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kupata chanjo  dhidi ya Ugonjwa wa polio.

Hata hivyo Mratibu Habibu aliongezea kwamba idadi ya timu za wachanjaji, watunza taarifa pamoja na wahamasishaji wamefikia idadi ya watu 647 katika Wilaya zote Saba huku idadi ya vibebea chanjo vinavyohitajika vikiwa 647 sawa na idadi ya wahusika.

Aidha chanjo hizo tayari zimekwisha sambazwa katika maeneo mbalimbali ya vituo vya Afya katika Halmashauri zote Saba huku mafunzo yanaendelea kutolewa kwa wachanjaji watunza takwimu na wahamasishaji. Aliendelea kufafanua Mwinory.

Awali akitoa maelezo juu ya Ugonjwa huo Habibu amesema polio inaenezwa kupitia njia ya haja kubwa  kwa mtu kula au kunywa  vitu ambavyo sio salama ambapo Ugonjwa huweza kumpata mtu yeyote kàtika umri wowote ila mtoto chini ya miaka mitano huathirika zaidi.

Naye Mkuu wa Wilaya Singida Mhandisi Pasksi Muragili ametoa wito kwa wananchi wote mkoani hapa kushiriki zoezi hilo la chanjo salama ya kuzuia Ugonjwa wa polio kwa watoto chini ya miaka mitano huku akiwataka wazazi wenye Tabia ya kuwaficha watoto kuacha Tabia hizo Mara moja.

Aidha ameitaka timu iliyoundwa kwa ajili ya uhamasishaji kutumia vyomba vya habari kama mkakati maalum wa kufikisha taarifa hizo kwa watu wengi na  kutumia taasisi za dini kufikisha ujumbe kwa waumini wao.

Hata hivyo Mhandisi Muragili akaelekeza kushirikishwa viongozi wa ngazi za vijiji na Kata kwa kuwa wao ndio waliopo karibu na watu.

Kikao kikiendelea



No comments:

Post a Comment