Sunday, April 03, 2022

Viongozi wa dini mkoani Singida waombwa kusaidia kutoa elimu ya Lishe katika Nyumba za Ibada

 

Viongozi wa dini mkoani Singida wameombwa kuisaidia jamii ya maeneo hayo kwa kutoa elimu ya Lishe katika Majumba ya Ibada  kwa watoto na mama wajawazito ili kupunguza tatizo la utapia mlo ambalo limekuwa likiwaathiri watoto wa umri wa chini ya miaka mitano kwa kiasi kikubwa mkoani hapo.

Akizungumza katika kikao kazi kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa  huo Kaimu Afisa Tawala Mkoa Beatusi Choaji amesema elimu kuhusu Lishe bado haijatolewa kwa kiasi cha kutosha na maana bado jamii inaathirika na swala la kuacha kula makundi muhimu ya vyakula, hivyo kuwaomba viongozi wa dini kusaidia kutoa elimu hiyo ili kubadilisha  Tabia ya ulaji kwa wananchi hao.

Kaimu RAS huyo amesema kwamba wakulima wa Mkoa wa Singida wanalima vyakula vingi vikiwemo viazi lishe  mahindi maharage na wanaongoza kwa ufugaji wa kuku wa kienyeji hivyo utapia mlo kwa kiasi kikubwa linaweza kusababishwa na kutowalisha vizuri watoto vyakula na sio kwamba hakuna vyakula.

Amewataka wataalamu wa Lishe mkoani hapo kutumia majukwaa mbalimbali kupeleka elimu ya Lishe kwa wananchi na kuhakikisha  katika Zahanati na vituo vya Afya wanakuwa na utaratibu wa kutoa elimu ya Lishe kwa kuwafuata watu majumbani na sio kuwasubiri Hospitalini wakiwa tayari wameshaathirika.

Akimalizia Kikao hicho Kaimu Katibu Tawala Mkoa akaagiza kuwakutanisha  Maafisa Lishe wa ngazi zote za Wilaya na Halmashauri ili kuja na mikakati mipya ya kupambana na tatizo la Lishe pamoja na kuwekana sawa kwenye zoezi uchukuaji wa takwimu za hatua za mapambano kwenye kutenga na kutumia bajeti zinazotengwa katika Halmashauri hizo.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa huo Victorine Ludovick akabainisha kwamba bado changamoto ya umbali kutoka vituo vya Afya na makazi ya wananchi imeonekana kuwa changamoto kwa kuwa wagonjwa wengi wanashindwa kufika vituo vya huduma kwa sababu ya umbali huo.

Hata hivyo amesisitiza kuchukua hatua za  kuongeza mbinu za uelimishaji kwa Jamii ili kuweza kutumia vyakula vinavyopatikana katika maeneo yao na kusaidia kukinga uwepo wa utapia mlo badala ya kujikita katika kutibu.

Kikao hicho kiliwahusisha wataalamu wa Lishe kutoka Sekta binafsi, Sekretarieti ya Mkoa, wawakilishi wa vyombo vya habari na viongozi wa dini.

No comments:

Post a Comment