MKUU wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge ameridhishwa na
kasi ya ujenzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Iramba
mkoani hapa ikihusisha ujenzi wa vituo vya afya, shule na visima
vya maji lengo likiwa ni kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi na kuondoa
msongamano.
Akiongea leo na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Iramba Rc Mahenge
ametaja miradi inayotekelezwa kwamba ni ujenzi wa shule ya Sekondari
Maluga inayotarajiwa kugharimu kiasi cha Tsh. Milioni 470, ujenzi wa
vituo vya Afya vinne (4) vya Tyegelo, Kisiriri, Mwanduigembe na Ndulungu
pamoja na ujezi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Sekondari
za Tulya na Kisiriri ambavyo kwa ujumla wake vinagharimu kiasi cha Tsh.
Bilion 1.525 zitokanazo na tozo ya miamala ya simu.
Aidha RC Mahenge akawataka wasimamizi na wahandisi wa miradi
mbalimbali wilayani hapo kuiga mifano ya miradi inaotekelezwa na Wakala wa
usambazaji wa maji Vijijini na usafi wa mazingira (RUWASA) ambapo
wamekuwa wakisimamia miradi yao kwa ufanisi na kuhakikisha thamani ya
fedha inaonekana.
Katika taarifa yao RUWASA imeonesha kwamba katika Wilaya ya Iramba
wana miradi mikubwa mitano (5) katika vijiji vitano vya Maluga,
Zinziligi, Kisiriri, wembere na Kaselya pamoja na uchimbaji wa visima
24 katika vijiji mbalimbali ambapo miradi yote inagharimu kiasi cha
Tsh.Bilion 3.304 na imetekelezwa kwa asilimia 70.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa huyo, DC wa Iramba Suleimani
Mwenda alisema Wilaya imepokea jumla ya Tsh.Bilion 1.119 kwa ajili ya Ujenzi wa
miradi ya maji katika vijiji vinne huku ikipokea jumla ya Tsh. Milioni 940 kwa
ajili ya Ujenzi wa shule mpya za Kata ya Maluga na Ndulungu.
Hata hivyo DC Mwenda akabainisha kwamba Wilaya ya Iramba
imepata fedha kiasi cha Tsh. Bilioni 1.473 zitokanazo
na ruzuku kutoka Serikali kuu ambapo zinatumika katika Ujenzi wa Kituo
cha Afya cha Mtoa na ukamishaji wa madarasa 10 ya shule za msingi.
Aidha fedha hizo zinatumika pia katika Ujenzi wa madarasa Sita
katika Shule za Sekondari sita pamoja na ukamilishaji wa vyumba 10 vya
Maabara katika Shule za Sekondari tano wilayani hapo aliendelea kusema DC
Mwenda.
MATUKIO KATIKA PICHA
Mradi wa Maji katika Kijiji cha Maluga wilayani Iramba
www.singida.go.tz
No comments:
Post a Comment