Vijana mkoani Singida wametakiwa kujiamini, kuonesha na
kuvitumia vipaji walivyonavyo katika kuleta ubunifu na ugunduzi wa mambo kwa
kuwa wengi wana vipaji lakini
hawajavitambua.
Akiongea katika Kongamano la maadhimisho ya 58 ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania lilofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha
uhasibu (NlT) uliyopo mkoani hapo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Gerry Muro amewataka
vijana kuhakikisha wanatumia akili zaidi kuliko elimu katika kutambua vipaji walivyonavyo
na kuchukua hatua.
Akieleza umuhimu wa vijana kutumia akili zaidi kuliko elimu
DC Muro amesema kwamba duniani wagunduzi wakubwa hawakutumia elimu lakini walitumia
akili na wakafika mbali hivyo kuwataka wajitume na waweze kutumia vipaji vyao kama
njia ya kupitisha elimu wanazopata.
Aidha DC Muro amebainisha kwamba kijana anayemaliza chuo na
kukaa mtaani akisubiri Serikali itoe ajira ni matokeo mabaya ya matumizi ya
vipaji kwa kuwa kila mmoja amepewa kipaji chake.
Amewataka vijana kujiunga katika vikundi na kuvisajili ili
waweze kupata mikopo kupitia asilimia Nne katika Halmashauri zao huku
akiwakumbusha Maafisa Maendeleo ya Jamii kuendelea kutoa msaada wa mawazo kwa
vijana wenye vikundi.
DC Muro ameendelea kusema kwamba huenda matumizi mabaya ya
simu janja ndio chanzo cha vijana kushindwa kufikiria vizuri namna ya kutatua
changamoto zinazowakabili ikiwemo ugunduzi wa vipaji vyao na namna ya kupata
mitaji na utajiri kwa ujumla.
Amewataka vijana kutumia Kongamano kuzitumia fursa ambazo
zimekuwa zikioneshwa katika mada mbalimbali zilizowasilishwa, na kila mwenye
kipaji kuanza kuzitumia.
Kwa upande wake Afisa Vijana Mmoa wa Singida na mratibu wa
Kongamano hilo Fredrick Ndahani amesema lengo la Kongamano hilo ni kuonesha
fursa za kiuchumi ambazo zimezunguka Mkoa wa Singida ili waweze kuzitumia na
kujikwamua katika maisha yao ya kila siku.
Aidha akieleza jitihada za Serikali katika Mkoa wa Singida
zakuwainua vijana amesema katika kipindi cha mwaka 2021/2022 Mkoa umetoa jumla
ya Tsh. Milioni 601.4 ikiwa ni mikopo iliyotolewa katika vikundi 133.
Amebainisha kwamba jumla ya ekari 23418 zimetengwa kwa ajili
ya vijana ili kufanya shughuli za uwekezaji na michezo katika Wilaya ya Manyoni
Ikungi Singida na Itigi.
Afisa vijana huyo wa Mkoa akawataka vijana kuacha kutumika katika matukio ya uvunjifu wa Amani na kujihusisha na mambo ambayo yatawajengea uaminifu mkubwa.
No comments:
Post a Comment