Saturday, April 23, 2022

Singida kutatua Mgogoro wa mashamba ya korosho uliodumu kwa miaka mitatu

Kamati zinazoshughulikia changamoto ya ugawaji wa mashamba ya korosho wilayani Manyoni zimepewa Siku Saba kuanza tarehe 25 April 2022  kugawa na kuwaonesha mashamba wakulima wa zao hilo lengo likiwa ni kuhakikisha ifikapo Octoba  2022 yawe yamekwisha safishwa na kilimo kimeanza.

Kauli hiyo imetolewa leo  na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.  Binilith Mahenge alipokutana na wakulima zaidi ya Mia na hamsini  katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Manyoni waliokuwa wakilalamikia mchakato wa ugawaji wa mashamba kugubikwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kukosa mashamba kwa wakulima waliolipia, mashamba kutosafishwa wakati yalishalipiwa na bàadhi ya wakulima walilipa fedha kwa muda mrefu lakini hawajaoneshwa mashamba yao.

RC Mahenge ameagiza kamati hizo kutumia Siku Saba kuanzia Siku ya tarehe 25 April kutambua majina ya wote wanaotakiwa kupatiwa mashamba na kuanza kuwaonesha mashamba yao huku akisisitiza kwamba hakuna mtu atakayepoteza haki yake.

Aidha ameagiza kuandaliwa andiko na mihtasari ya mikutano inayofanyika ili kusaidia usimamizi wa mashamba hayo na kurahisisha ufuatiliaji wakati wanapokuja viongozi wapya.

RC Mahenge amesema utaandaliwa utaratibu mzuri wa mawasiliano baina yao na wenye mashamba ili kuondoa changamoto hizo ambazo zimedumu kwa miaka zaidi mitatu.

"Changamoto zote zilizotokea mpaka kusababisha migogoro katika ugawaji wa mashamba na kutuchelewesha  kwa miaka mitatu limesababishwa na ufuatiliaji na usimamizi mbaya uliofanywa na bàadhi ya Maafisa wa Serikali, lazima tutengeneze utaratibu mzuri utakaosaidia kuendeleza zao la korosho mkoani hapa" alibainisha Dk. Mahenge.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko amesema wamedhamiria kuondoa changamoto zilizojitokeza na watahakikisha kwamba ifikapo Oktoba 2022 mashamba yote yatakuwa yamekamilika ili kuongeza uzalishaji wa Korosho na kuongeza mapato ya Wilaya hiyo na Mkoa kwa ujumla.

Hata hivyo RAS huyo amewataka wakulima  kuiamini timu inayoshughulikia matatizo ya  changamoto hizo na kutoa ushirikiano pale utakapohitajika ikiwemo ukaguzi wa nyaraka za malipo na mahitaji mengine.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko akizungumza wakati wa kikao hicho

Aidha kwa kuanza kubadisha utaratibu RAS akabadilisha Mratibu wa Awali na kumteua Bwana Lucas Mkuki Afisa kilimo  kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuendeleza  uratibu wa ugawaji wa mashamba ambapo atafanya kazi kwa kushirikiana na kamati zitakazokuwepo.

 Akizungumza kwa niaba ya wakulima wengine Abdala Mbonde ameishukuru Serikali ya Mkoa kwa maamuzi yao ya kuhakikisha  changamoto zinatatuliwa na kilimo cha korosho kinaanza.

 Mbonde ameshauri kuwa kamati itakayoundwa ihakikishe haki inatendeka kwa wakulima hao wa zao la korosho ili waweze kuendelea na uwekezaji huo katika kilimo hicho kwalengo la kujikwamua kiuchumi.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA WAKATI WA KIKAO




Wadau mbalimbali wa kilimo cha korosho wakizungumza wakati wa kikao


Kikao kikiendelea

Timu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida ikiwasikiliza wakulima walio na changamoto mbalimbali za mashamba ya korosho ili kuzitatua.

No comments:

Post a Comment