Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge leo ameliapisha
Baraza jipya la ardhi la wilaya ya Mkalama baada ya viongozi hao kuteuliwa na
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kushughulikia migogoro
mbalimbali ya ardhi wilayani hapo.
Akiongea baada ya kuwaapisha, RC Mahenge akawataka wajumbe
hao kuanza kazi kwa kusoma mihutasari yote ya mabaraza ya nyuma ili waweze
kupata uzoefu kabla ya kuanza kutatua kesi zinazowakabili wananchi wa Mkalama.
Aidha amelitaka Baraza hilo kufanya kazi kwa weledi mkubwa katika kuendesha kesi za ardhi na kufanya maamuzi ya busara pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa, zawadi na takrima kwa kuwa vinaweza kuathiri maamuzi sahihi ya baraza.
Hata hivo RC Mahenge akatoa malekezo kwa baraza hilo
kuhakikisha wanapunguza au kuondoa kabisa kero na migogoro ya ardhi kwa
kuhakikisha wanasikiliza pande zote na kuyatembelea maeneo yenye changamoto
badala ya maelezo peke yake huku wakikumbushwa kutofautisha kesi za mashamba au
ardhi na kesi za wizi wa aina yeyote ile.
“Mfanye maamuzi baada ya kujiridhisha kwa sababu kesi za
ardhi nyingi zimekuwa ni za kifamilia lakini pia kuna tofauti kubwa kati ya
kesi za mashamba au ardhi na kesi za wizi wa kuku, ninaomba mjifunze kwa
wenzenu mshirikiane na vyombo mbalimbali mtakavyoona vinaweza kusaidia lakini
mhakikishe haki inatamalaki Mkalama”. Alisema RC Mahenge.
Akimalizia hotuba yake Mkuu wa Mkoa akalitaka Baraza hilo
kutafuta namna ya kutatua changamoto ya ardhi kwa vijana kwa sababu familia
zinapoingia katika migogoro ya hiyo wanaoteseka na kuingia hasara ni Vijana .
“Nyuso zenu zinaonesha nyie ni watu waaminifu na wenye
weledi mkubwa hivyo katika kutekeleza majukumu yenu mapya mfikirie njia nzuri
ya kuwasaidia vijana ambao wamekuwa wakiathirika sana na migogoro ya aridhi
hasa ile ya kifamilia”. Alisema RC Mahenge.
Mwisho wa Hotuba yake RC Mahenge akabainisha kwamba ardhi ni
sehemu nyeti kwa wanadamu na wanyama
hivyo kazi hiyo inaweza kusaidia ustawi
wa jamii au kuharibu kabisa ambapo alielekeza kwamba utatuzi wa migogoro
ufanyike kwa weledi mkubwa .
Naye DC wa Mkalama Sophia Kizigo akilipongeza baraza hilo
kwa kupata uteuzi huku akieleza umuhimu wake katika kutatua matatizo ya
wananchi wa Mkalama ambao wengi wao wamekuwa wakipoteza haki zao kwa kushindwa
kusafiri umbali mrefu kusikiliza kesi zinazohusu ardhi zao.
Amesema wananchi wa Mkalama walikuwa wanalazimika kwenda mpaka Wilaya ya Iramba Mkoani hapo kusikiliza mashauri yao kwa kuwa huko ndipo baraza la ardhi lilipokuwa likipatikana na kulitaka kurejesha Imani za wananchi hao ambao haki zao zilipotea.
Aidha DC Kizigo akaeleza kwamba kiapo walichopata ni ulinzi
kwao ambapo wanatakiwa kuepuka kupokea rushwa na kuhakikisha hawachonganishi
wananchi .
Hata hivyo DC huyo akamalizia hotuba yake kwa kuahidi
ushirikiano mkubwa kwa baraza hilo huku akikumbusha kwamba litapimwa utendaji wake kwa kipindi
kisichozidi miezi sita na kuona kama linawasaidia wananchi kutatua migororo au
inaongezeka.
Awali akitoa salamu zake Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Mkalama James Mkwega pamoja na pongezi
kwa baraza hilo akawataka kumtanguliza Mwenyezimungu katika shughuli zao ili
aweze kuwangoza katika kutatua matatizo ya ardhi ambayo yamekuwa mengi wilayani
humo.
Mwenyekiti Mkwega akaendelea kueleza kwamba kazi kubwa
imefanyika ya kupata baraza hilo ambapo kilikuwa ni kilio cha Madiwani wote
kutokana na malalamiko ya wananchi kupoteza haki zao .
Kupata baraza ni jambo moja na huduma za baraza ni jambo la
pili, ni matumaini yetu sisi wanamkalama kwamba huduma yenu itatusaidia kupata
haki zetu, James Mkwega.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza hilo Baraka Shuma kwa
niaba ya wajumbe akatoa shukrani kwa kuteuliwa katika nafasi hiyo huku akiahidi
kutekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha wanawasaidia wananchi
wa wilaya hiyo.
Shughuli hiyo ya uapisho ilihudhuriwa na Mkuu wa mkoa Singida, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba na Mweyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo ambapo Wajumbe walioapishwa ni Charles Jilangi, Kitundu Emanuel Kitundu, Hamisi Igimbi Salum na Zulfa Suphian Mvungi.
No comments:
Post a Comment