Wananchi wa Mkoa wa Singida wametakiwa kuendelea kukarabati majengo ya zamani ya shule na vituo vya Afya vilivyopo mkoani hapo ili majengo hayo yaweze kuendelea kutumika kwa matumizi mbalimbali.
Wito huo umetolewa leo na Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi CCm Mkoa wa Singida Juma Kilimba wakati alipokuwa katika
ziara ya kukagua na kupokea miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Manyoni na
Itigi.
Kilimba amesema kwamba Serikali imejenga Madarasa mapya 632
kupitia fedha za miradi ya maendeleo kwa Mkoa huo hivyo kuwataka Madiwani na
viongozi wa vijiji na kata kusaidia usimamizi wa matumizi ya majengo hayo na
kuwataka kuhakikisha ukarabati unafanyika katika madarasa ya zamani ili yaweze
kuendelea na matumizi.
“Haina maana kwamba kwa kuwa tumepata madarasa mapya mengine
ya zamani tuyaache bila kuyakarabati, viongozi wa vijiji na kata kwa
kushirikiana na madiwani kuona namna ya kukarabati majengo ambayo yanaonekana
kuwa yamechoka ili yaendelee kutumika”. Alisema Kilimba
Akitolea mfano wa mijadala iliyoibuliwa katika kikao cha
ushauri wa mkoa (RCC) kilichofanyika hivi karibuni mkoani hapo Juma Kilimba
amesema mkoa umetafiti mbinu mbalimbali
za kuimarisha viwango vya ufaulu, mbinu za kutumia TEHAMA katika kuondoa changamoto ya uhaba wa walimu
hivyo majengo hayo yatakuwa na kazi kubwa
endapo yatakarabatiwa.
Akiendelea na ukaguzi wa miradi mbalimbali Mwenyekiti huyo
akaishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya mama Samia Suluhu Hassani kwa kutoa
kiasi kikubwa cha fedha ambapo katika kipindi cha mwaka 2022 wameweza kujenga
miundombinu ya mabomba na kuchimba visima, ujenzi wa barabara za vijijini
pamoja ujenzi wa vituo vya Afya.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo Dk. Binilith Mahenge
akawataka ruwasa kuhakikisha wanajenga miundombinu ya maji iliyo imara ili
kiuwasaidia wananchi kwa muda mrefu huku akiwakumbusha wataalamu hao
kuhakikisha wanawasaidia wananchi waweze kuvuta maji majumbani mwao.
Aidha RC Mahenge akawataka wasimamizi wa miradi mbalimbali
Mkoani hapo kuhakikisha kwamba fedha walizopewa zinatumika kama ilivyokubaliwa
na kuleta tija kwa wananchi kwa kuwa lengo la serikali ni kuwanufaisha wananchi
wake.
Wakiendelea na ukaguzi katika hospitali ya wilaya ya Manyoni Mwenyekiti wa halmashauri Jumanne Mlagaza pamoja na kuishukuru serikali kwa kuwapata fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo, akamuomba mwenyekiti kusaidia wazo la kupata eneo la kujenga hospitali kubwa ya wilaya kwa kuwa eneo walilonalo kwa sasa ni dogo na halina miundombinu mizuri ya barabara na majengo ya kutosha.
Hata hivyo Jumanne akaendelea kusema kwamba miradi yote inayotekelezwa katika Halmashauri
ya Manyoni inategemewa kukamilika kwa wakati pamoja na uwepo wa changamoto za
mvua na baadhi ya vitu kupanda bei.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri wa Wilaya ya Manyoni
Melckzedek Humbe akitoa taarifa ya miradi yote wilayani hapo amesema
halmashauri imepokea jumla ya Tsh. Bilioni 5.6 ambapo kati ya hizo Tsh.7.3 sawa
na asilimia 75.9 ya fedha zilizotengwa.
Aidha Humbe akasema
kwamba miradi iliyotekelezwa ni
ukamilishaji wa vyumba vya maabara katika shule za sekondari, uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali na
utekelezaji wa shughuli za TASAF.
Ziara hiyo inaendelea kesho katika wilaya ya Iramba na Ikungi baada ya leo kufanyika katika wilaya ya Manyoni na Halmashauri ya Itigi huku kikosi kingine kikendeleza na ziara hiyo wilaya ya Mkalama.
No comments:
Post a Comment