Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amewataka wananchi wa kijiji cha Msikii Kata hiyo na Munkhola Kata ya Mgori wilaya Singida vijijini kutumia njia ya majadiliano na maridhiano katika kutatua mgogoro wa matumizi ya ardhi unaowakabili.
Dkt. Mahenge ameyasema hayo hivi karibuni wakati alipofanya ziara ya kujifunza na kujionea eneo lenye mgogoro baina ya vijiji hivyo ambapo kijiji cha Munkhola wanataka eneo hilo libaki kama hifadhi ya Msitu wakati kijiji cha Msikii wakita litumike kwa ajili ya kilimo.
Aidha Dkt. Mahenge akiwa eneo hilo akawataka madiwani wa Munkhola na Msikii kukutana ili kujadili kwa kina athari zinazoweza kutokea endapo eneo hilo likitumika kwa kilimo au kwa hifadhi ya msitu ambapo watashirikiana na kamati iliyoundwa ili kupata suluhisho.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa akawasihi wananchi wa vijiji hivyo
kuendelea kutunza amani utulivu na mshikamano wakati viongozi wao wakitafuta suluhisho
la mgogoro huo huku akisisitiza mazao na miti iliyopandwa eneo hilo kuendelea
kubaki mpaka muafaka utakapopatikana.
“Sitapenda kusikia watu wamegombana au miti na mazao yameng’olewa wakati Serikali ipo, atakaye thubutu kuvunja amani sitakuwa na urafiki katika hilo.” Alisisitiza Dkt. Mahenge
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Singida vijiji William Nyalandu akawasisitiza viongozi wa
vijiji hivyo kufuata maagizo yaliyotolewa na Serikali ya kuhakikishi amani na
utulivu vinakuwepo.
Hata hivyo Nyalandu akasisitizia kwamba mazao yaliyopo kutong’olewa na viongozi wahakikishe hakuna mkulima mwingine atakayeanzisha shamba jipya katika eneo hilo mpaka hapo Serikali itakapotoa muongozo.
Diwani wa Kata ya Munkhola Mhe. Dhuma Said akamuhakikishia RC Mahenge kwamba mgogoro huo utaisha kwa kutumia mijadala ya kawaida baina yao viongozi na hauwezi kwenda hatua za juu.
Hata hivyo Diwani huyo alieleza kwamba shughuli za kilimo na ufugaji zinazofanywa katika hifadhi ya msitu huo zinahatarisha maisha ya wananchi wanaozunguka eneo hilo na Mkoa kwa ujumla kwa kusababisha mmomonyoko wa udongo, jangwa na ukosefu wa mvua.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Msikii Mhe. Mchaga Mtegagufa akatumia muda huo kumueleza Mkuu wa Mkoa kwamba kutokana na mgogoro huo ng’ombe Sita kutoka katika kijiji cha Msikii wamekamatwa, majembe Mawili yakukokotwa na ng’ombe hayajulikani yalipo mpaka sasa.
Hata hivyo Diwani Mchaga akamuomba Mkuu wa Mkoa waachiliwe
huru watu wawili wa kijiji hicho waliokamatwa ambapo Mkuu wa Mkoa alimwagiza
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa kuwaachia huru watu hao kwakuwa viongozi watakutana
kwa ajili ya muafaka.
Ziara hiyo iliwahusisha Kamati ya Usalama ya Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Mwenyekiti wa Halmashauri, Kamati maalum ya utatuzi wa migogoro na viongozi wa Chama cha Mapinduzi.
No comments:
Post a Comment